Hatua ya Marekani kusitisha msaada wa kigeni umeathiri pakubwa mpango wa utafiti wa chanjo ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini Afrika Kusini, hatua yenye athari kubwa kote duniani na hususan barani Afrika.
Ilikuwa imesalia wiki moja tu kabla ya wanasayansi wa Afrika Kusini kuanza majaribio ya kimatibabu ya chanjo ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), na matumaini yalikuwa makubwa ili kufikia hatua nyingine ya kujaribu kukabiliana na moja ya magonjwa hatari zaidi katika historia.
Na ndipo barua pepe iliwasili ikiwaamuru wanasayansi hao kusitisha shughuli zote. Marekani chini ya utawala wa rais Donald Trump ulikuwa umesitisha ufadhili wake wote katika mradi huo wa majaribio. Taarifa hizo ziliwakwaza mno watafiti, wanaoishi na kufanya kazi katika eneo ambalo watu wengi wanaishi na VVU kuliko mahali pengine popote duniani.
Mradi huo wa utafiti unaoitwa BRILLIANT, ulikusudiwa kuwa wa hivi punde zaidi unaotumia mchanganyiko wa tofauti za vijinasaba na utaalamu wa kina wa eneo hilo ili kuwanufaisha waathirika wa virusi vya Ukimwi kote duniani.
Lakini dola milioni 46 kutoka Marekani zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mradi huo zilitoweka, kufuatia kusitishwa kwa misaada ya kigeni na mfadhili mkuu duniani mapema mwaka huu, hasa kutokana na hatua ya Rais Donald Trump kutangaza kuwa kwa sasa anazingatia kwanza vipaumbele vya taifa lake.
Afrika Kusini yaathirika mno na hatua hiyo
Afrika Kusini imeathirika kwa kiasi kikubwa na hatua hiyo hasa baada ya Trump kutoa madai yasiyokuwa na msingi kwamba utawala umekuwa ukiwalenga jamii ya walio wachache wa Afrika Kusini, wazungu. Nchi hiyo imekuwa ikipokea takriban dola milioni 400 kwa mwaka kupitia mashirika ya misaada ya USAID na PEPFAR yanayolenga kukabiliana na VVU. Lakini sasa misaada yote hiyo imetoweka.
Glenda Grey, ambaye anaongoza mradi huo wa Brilliant, amesema bara la Afrika limekuwa na jukumu muhimu katika kufikia mafanikio ya dawa za VVU , lakini kusitishwa kwa msaada wa Marekani kunatishia uwezo wa bara hilo kuendelea na jukumu hilo katika siku zijazo.
Maendeleo makubwa yaliyoshuhudiwa ni pamoja na majaribio ya kimatibabu ya dawa aina ya "lenacapavir", chanjo pekee duniani ya kuzuia kuenea kwa VVU ambayo muathirika huchomwa mara mbili kwa mwaka. Chanjo hiyo iliidhinishwa kwa matumizi rasmi hivi majuzi na mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani (FDA), na utafiti wake uliwahusisha vijana wa Afrika Kusini.
"Tunafanya majaribio vizuri zaidi, kwa haraka na kwa bei nafuu kuliko mahali pengine popote duniani, na hivyo bila Afrika Kusini kuwa sehemu ya programu kama hizi, bila shaka dunia itaathirika zaidi." Grey alisema akisisitiza kuwa hayo ni maoni yake. Alibainisha kuwa wakati wa janga la UVIKO-19, Afrika Kusini ilichukua jukumu muhimu kwa kuzijaribu chanjo za Johnson & Johnson na Novavax, uchunguzi uliopelekea wanasayansi wa Afrika Kusini kugundua aina nyingine ya virusi hivyo.
Grey anasikitika kushuhudia katika taifa ambalo karibu asilimia 46 ya vijana hawana ajira, maabara zikiwa tupu huku maelfu ya wanasayansi wakiachishwa kazi ikiwa ni pamoja na timu ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Witwatersrand iliyokuwa sehemu ya kitengo kinashiriki mpango wa majaribio wa kutengeneza chanjo hiyo ya kuzuia VVU. Ameongeza pia kuwa hatua hiyo inawanyima fursa ya kushirikiana na wanasayansi wengine wa Afrika.
Profesa Abdullah Ely aliyekuwa akiongoza timu hiyo ya watafiti amesema kazi waliyokuwa wakiifanya ilikuwa imeanza kuonyesha matokeo chanya yanayodhihirisha kuwa chanjo hizo zilikuwa na uwezo wa kutoa kinga, lakini akasikitika kuona kwamba juhudi zote hizo sasa zimelazimika kusitishwa.
BRILLIANT sasa inahangaika kutafuta fedha za kuokoa mradi huo .Ununuzi wa vifaa muhimu umesimama na idara ya afya ya Afrika Kusini inasema watafiti wapatao 100 wa mradi huo na wengine wanaohusishwa na miradi ya VVU wameachishwa kazi. Ufadhili wa mpango wa kuwahusisha wanafunzi wanaosomea udaktari katika majaribio ya miradi hiyo uko pia hatarini.
Serikali ya Afrika Kusini inakadiria kuwa miradi ya wanasayansi kuhusu magonjwa ya VVU na hata kifua kikuu itapoteza karibu dola milioni 107 kutokana na hatua ya Marekani kusitisha misaada ya kigeni, huku ikisisitiza kuwa itakuwa vigumu kupata fedha zitakazoweza kuziba pengo la ufadhili wa Marekani.
Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kuongezeka
Hatua hiyo itapelekea pia dawa za kupunguza makali ya VVU kuwa vigumu kupatikana. Angalau maafisa wa afya 8,000 nchini Afrika Kusini waliokuwa wakifanya kazi katika mpango wa VVU tayari wamefutwa kazi, kulingana na serikali. Pia, timu ya wauguzi waliokuwa wakikusanya data na kufuatilia hali jumla ya wagonjwa ikiwa ni pamoja na washauri wa ugonjwa wa VVU ambao wangeliweza kuwafikia wagonjwa walio katika mazingira magumu ya vijijini pia wametoweka.
Katika ziara yake nchini Afrika Kusini mwezi Juni, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa, UNAIDS Winnie Byanyima alitambua kuhusu dharura iliyopo na maisha ya mamilioni ya watu yaliyokuwa hatarini kutokana na hatua hiyo hasa ikizingatiwa kuwa miradi ya utafiti na huduma za afya nchini Afrika Kusini na kote barani Afrika ikifungiwa ufadhili.
Nchi nyingine ambazo zilikuwa zinategemea pakubwa ufadhili wa Marekani zikiwemo Zambia, Nigeria, Burundi na Ivory Coast tayari zinapambana ili kukidhi mahitaji yao kwa kutumia uwezo wao wa ndani, alisema Bi Byanyima lakini akasisitiza kuwa wanachokitoa hakitaweza kufidia ufadhili wa Marekani.
(Chanzo: AP)
image quote pre code