Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF, afya duniani WHO, linalohudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA na wizara ya afya ya Palestina wamezindua kampeni maalum ya chanjo, lishe na ufuatiliaji wa ukuaji wa watoto katika Ukanda wa Gaza, lengo likiwa ni kuwafikia watoto 44,000 waliokosa huduma muhimu za afya kutokana na vita vilivyodumu kwa miaka miwili.
Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo imeeleza kuwa kampeni hiyo itafanyika kwa awamu tatu, Kati ya mwezi huu wa Novemba 2025 mpaka mwezi Januari 2026 ikilenga kuwapatia watoto chanjo dhidi ya magonjwa hatari kama surua, rubella, kifaduro, dondakoo, pepopunda, homa ya ini, kifua kikuu, polio na nimonia.
Awamu ya kwanza itaanza tarehe 9 hadi 18 Novemba 2025. Awamu ya pili na ya tatu za kampeni zinatarajiwa kufanyika Desemba 2025 na Januari 2026, zikiwa na lengo la kurejesha kiwango cha chanjo kama kabla ya vita.
Kabla ya vita, Gaza ilikuwa na kiwango cha chanjo cha zaidi ya asilimia 98 kwa watoto, lakini sasa kiwango cha chanjo kimeshuka chini ya asilimia 70.









image quote pre code