Hulay Damba,ni mama mwenye umri wa miaka 55, kwa miaka mingi akitekeleza vitendo vya ukeketaji au FGM kwa wasichana katika jamii yake huko Basse, Gambia.
Jukumu lake kama ngariba lalirithi kutoka kwa nyanya yake. “Ndivyo nilivyofundishwa,” ameeleza. Licha ya miaka ya juhudi za uhamasishaji nchini Gambia, viwango vya ukeketaji wa wanawake na wasichana bado ni vya juu, hata kwa vizazi vya sasa.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021, za Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA karibu robo tatu ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wamekeketwa nchini Gambia kiwango ambacho ni sawa na kile cha wanawake wa kizazi kilichowatangulia wenye umri wa miaka 45 hadi 49.
Utafiti wa akina mama uliofanywa pia unaonesha matokeo yenye mchanganyiko wakati wanawake wenye mabinti wenye umri wa miaka 25 na chini ya hapo waliulizwa kama mabinti wao wamekeketwa asilimia 54 walisema hapana.
Lakini asilimia 22 walisema kwamba binti zao sio tu wamekeketwa bali walikeketwa kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.
Kubadilisha mawazo
Nchini Gambia, wasichana wengi wanaokeketwa hukatwa sehemu zao za siri wakati wa taratibu hizo za kijadi. Takriban asilimia 12 hushonwa kabisa.
Karibu wote hupitia ukeketaji huu mikononi mwa wakunga wa jadi na mangariba kama Bi. Damba.
Bi. Damba amewahi kupata kipato kizuri cha msimu kwa kufanya kazi ya ungariba. “Niliamini ilikuwa ni heshima,” amelieleza shirika la UNFPA.
Yote yamebadilika miaka sita iliyopita, alipoanza kuhudhuria mafunzo kadhaa yaliyoongozwa na shirika lisilo la kiserikali la Tostan kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Italia (AICS) kupitia UNFPA, kuhusu madhara ya muda mrefu ya ukeketaji ambayo yanaweza kujumuisha kutokwa na damu nyingi, maambukizi, na hata kifo.
“Kwa kutazama ya nyuma, natamani ningejua kile ninachojua sasa,” anasema Bi. Damba.
Leo hii, Bi Damba anaongoza harakati za kukomesha kazi hiyo ya ukeketaji pamoja na akina mama wenzake na vijana.
“Sasa natumia sauti yangu kuelimisha,” anasema, “kwa sababu kila msichana anastahili kukua akiwa salama na kamili.”
Madhara katika wakati wa kujifungua
Fatou amezungumza na UNFPA akiwa katika wodi ya uzazi kwenye Hospitali ya Wilaya ya Basse. Akiwa na miaka 16 tu, akimshika mtoto mchanga wa kike mikononi mwake, akiugua kutoka katika kujifungua kwa ugumu baada ya kukeketwa.
Ujauzito wake ulihatarisha maisha yake na ya mtoto wake. Kwa bahati nzuri, mkunga aliweza kuingilia kati na kumsaidia. Hili ni jambo ambalo linajulikana kuongeza kwa kiasi kikubwa hatari za uzazi.
Hospitali hiyo ni sehemu ya mtandao unaokua wa vituo vya afya vinavyoshiriki katika mpango wa UNFPA, unaofadhiliwa na mradi wa AICS, kwa msaada wa ziada kutoka China Aid, unaotoa mafunzo maalum kwa watoa huduma za afya ili kushughulikia madhara ya ukeketaji, pamoja na huduma nyingine muhimu za afya ya uzazi.
Hata hivyo, bado hatua zaidi zinahitajika.
Mwaka jana, wabunge walijaribu bila mafanikio kuhalalisha ukeketaji wa wanawake, ambao umepigwa marufuku nchini Gambia tangu mwaka 2015. Wasichana, wakiwemo watoto wachanga, bado wanakumbwa na ukeketaji na kupata madhara yake.
Si ajabu kuwa ukeketaji hufanywa na wanawake wakubwa, anasema Fatou Baldeh, mwanzilishi wa shirika la Women in Liberation and Leadership.
“Wanawake bado ni waathirika na pia watekelezaji wa mila hii yenye ukatili mkubwa inayojaa ubaguzi wa kijinsia,” anasema.
“Wanawake hawa si watendaji tu ni matokeo ya mfumo unaofundishwa tangu kuzaliwa kwamba maumivu na kujitoa mhanga ni sehemu ya kuwa mwanamke shupavu.”
Kile kinachohitajika, ameongeza, ni juhudi za “kubomoa mienendo inayowasukuma wanawake kutekeleza kitendo hiki.”
Sasa kizazi kipya cha wanaharakati kinainuka kupambana na hali hiyo. Ramata Baldeh, msichana mwenye umri wa miaka 18, alikeketwa akiwa mdogo lakini anasema ukeketaji utaishia kwake.
“Ikiwa nitapata binti siku moja, sitaruhusu kamwe apitie mateso niliyopitia,” anasema. “Nataka aende shule ili aweze kutimiza ndoto zake na achague njia yake mwenyewe.” Via UN.
image quote pre code