Watu 32 wamepoteza maisha baada ya mgodi wa kobalti kuporomoka katika eneo la uchimbaji madini la Kalando, katika machimbo ya Mulondo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ajali hiyo ilitokea baada ya milio ya risasi inayodaiwa kuzuka kutoka kwa wafanyakazi wa usalama waliokuwa wakilinda eneo hilo, na kusababisha wachimbaji kutumbukia kwenye mgodi wa wazi.
Akizungumzia tukio hilo, siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Mkoa wa Lualaba, Roy Kaumba Mayonde, alisema, "Licha ya marufuku rasmi ya kuingia kwenye eneo hilo kutokana na mvua kubwa na hatari ya maporomoko ya ardhi, wachimbaji haramu walilazimisha kuingia kwenye machimbo hayo."
Aliongeza kuwa "kuvuka kwa haraka kwa wachimbaji" kulisababisha kuanguka kwa daraja la muda ambalo walikuwa wamejenga ili kuvuka mtaro uliofurika.
Mamlaka zinasema hadi sasa miili 32 imepatikana huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea. Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha miili ya wachimbaji iliyopatikana kutoka eneo la tukio huku wenyeji wakitazama kwa mshangao.
Mamlaka katika taarifa yao wamewasihi wachimbaji wadogo kuchukua fursa ya serikali ya mafunzo mbadala katika biashara ya kilimo ili kuepuka kujirudia kwa misiba kama hiyo wanapojihusisha na shughuli haramu za uchimbaji madini.
Ajali za uchimbaji madini si jambo geni nchini DRC, ambapo inakadiriwa kuwa watu milioni 1.5 hadi 2 hufanya kazi katika migodi ya madini isiyodhibitiwa ambayo inakidhi mahitaji ya kimataifa ya shaba, kobalti na madini mengine.









image quote pre code