Mafuriko Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika yaathiri watu 637,000
Mafuriko Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika yaathiri watu 637,000
IOM na Shirika la Msalaba mwekundu Kenya, kwa mchango wa ukarimu kutoka Japani wanasaidia watu waliohamishwa makazi yao Tana River, Kenya kwa malazi na vifaa muhimu vya nyumbani.
Wiki za mvua kubwa na mafuriko huko Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kumechochea ukimbizi ambapo mamia ya maelfu ya watu wamefurushwa makwao huko Burundi, Kenya, Rwanda, Somalia na Tanzania ambapo Umoja wa Mataifa unasema hadi tarehe 3 mwezi huu wa Mei, jumla ya watu 637,000 wameathiriwa, 234,000 kati yao hao wamelazimika kukimbia makwao.
Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limetoa takwimu hizo likinukuu ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, huku ikisema kuwa idadi inazidi kuongezeka kila uchao.
IOM kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na Nairobi, Kenya inasema mvua hizo za masika zimesababisha mafuriko makubwa, maporomoko ya udongo na kuharibu miundombinu muihmu kama vile barabara, madaraja na mabwawa ya maji.
IOM na Shirika la Msalaba mwekundu Kenya, kwa mchango wa ukarimu kutoka Japani wanasaidia watu waliohamishwa makazi yao Tana River, Kenya kwa malazi na vifaa muhimu vya nyumbani.
Mkurugenzi wa IOM Kanda ya Afrika MAshariki na Pembe ya Afrika Rana Jaber anasema mafuriko hayo ya kipekee na yaliyosababisha uharibifu yameibua ukweli mchungu wa mabadiliko ya tabianchi, kwa kusababisha vifo na kufurusha watu makwao, watu ambao sasa wanakabiliwa na kazi kubwa ya kujijenga upya huku hali zao zikizidi kuwa taabani.
Ni kwa mantiki hiyo anaesema katika nyakati hizi muhimu, wito wa IOM unasalia kuchukuliwa kwa hatua endelevu na za dharura za kutatua ukimbizi wa binadamu unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi.
Pamoja na kushirikiana na serikali na wadau kusambaza misaada ya hali na mali ya kuokoa maisha ikiwemo fedha taslimu kwa walioathiriwa huko Burundi, Kenya, Somalia, Ethiopia na Tanzania, IOM inasema mjadala ujao huko Ujerumani kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC ni dhahiri shairi kuwa mazungumzo kuhusu tabianchi lazima yazingatie ukimbizi utokanao na janga hilo.
Afrika inaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi licha ya kuchangia asilimia 4 pekee ya hewa chafuzi duniani.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!