Ticker

6/recent/ticker-posts

Fahamu Virusi vinavyojificha ndani ya Utumbo wako



Fahamu Virusi vinavyojificha ndani ya Utumbo wako

Microbiome - ni makundi ya bakteria na aina nyingine ndogo ndogo ya vidudu ambavyo huishi katika matumbo yetu. Imebainika kuwa bakteria hao wana virusi ambavyo vipo ndani na nje yao - na vina faida kwao na kwetu sisi.

Kuna mabilioni, labda hata trilioni za virusi hivi, vinavyojulikana kama bacteriophages au kwa jina jingine phages, ndani ya mfumo wa usagaji chakula wa binadamu.

Breck Duerkop, mtaalamu wa bakteria katika Chuo Kikuu cha Colorado Anschutz, anasema watafiti wanaamini ikiwa madaktari wanaweza kuvipata virusi sahihi, vinaweza kuboresha afya ya binadamu.

"Kutakuwa na virusi vizuri na virusi vibaya," anasema Paul Bollyky, daktari wa magonjwa ya kuambukiza na mtafiti katika taasisi ya Stanford Medicine.

Lakini kwa sasa, bado haijabainika ni virusi vingapi hukaa kwenye tumbo. Vilevile, kuna virusi vingine bado havijatambulika. Sehemu kubwa ya utafiti wa sasa wa virusi ni kutambua virusi hivi na bakteria wanaoishi nao.

“Aina zao ni za kushangaza," anasema Colin Hill, mwanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Cork huko Ireland. Wanasayansi hupata virusi kutoka katika sampuli za kinyesi cha binadamu.

Virusi hutofautiana sana kutoka kwa mtu mmoja hadi mtu mwingine. Pia hubadilika kulingana na umri, jinsia, chakula na mtindo wa maisha, kama Hill na wafanyakazi wenzake walivyoeleza katika utafiti wa mwaka 2023.

Ingawa virusi huambukiza bakteria na wakati mwingine huwaua, uhusiano wa bakteria na virusi bado ni mgumu kuuelewa.

"Tulikuwa tukifikiri kwamba virusi na bakteria wanapigana," anasema Hill, "lakini sasa tunajua kwamba wanaishi pamoja na ni washirika."

Manufaa ya virusi

Fahamu kwamba; Kila mmoja wetu ana virusi vya kipekee vinavyoingiliana kila mara na bakteria wa utumbo

Virusi vinaweza kutoa manufaa kwa bakteria kwa kuleta jeni mpya. Wakati chembe za virusi zinapokusanyika ndani ya bakteria, kirusi huyo anaweza kuingiza jeni za bakteria kwenye ganda lake la protini pamoja na jeni zake mwenyewe.

“Baadaye, huzifanya jeni hizo kuwa jeni mpya, ni jeni zilizohamishwa kwa bahati mbaya na zinaweza kusaidia,” anasema Duerkop.

Virusi huwaweka bakteria katika hali nzuri, anasema Hill. Bakteria wanaweza kuwa na hadi aina kumi na mbili za kinga. Kinga tofauti zina faida tofauti; kuepuka mfumo wa kinga mwili au kukaa kona tofauti ya mfumo wa utumbo.

Hill anasema, bakeria lazima kila wakati wabadilishe kinga zao ili kukwepa virusi vinavyotambua kinga moja tu. Matokeo yake, wanakuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto mpya.

Virusi pia huzuia idadi ya bakteria wasizidi kupita kiasi. Utumbo ni mfumo wa ikolojia, kama misitu, na virusi ni wawindaji wa bakteria, kama mbwa mwitu na wawindaji wengine.

Utumbo unahitaji virusi kama vile msitu unavyohitaji mbwa mwitu. Wakati mahusiano hayo yanapobadilika, ugonjwa unaweza kutokea.

Watafiti wameona mabadiliko ya virusi kwa watu wenye ugonjwa wa matumbo (IBS), kama ugonjwa wa kuharisha na saratani ya utumbo mkubwa - mfumo wa ikolojia wa mtu aliye na shida hizo mara nyingi huwa tofauti.

Hill anasema, wanasayansi wanatafuta virusi ambavyo vinaweza kutumiwa kimatibabu dhidi ya bakteria wanaosababisha vidonda vya tumbo.

“Nadhani, tunapaswa kushukuru kwa matrilioni ya virusi vinavyosimamia mfumo wa ikolojia ya utumbo. Bila wao, aina fulani ya bakteria zinaweza kutawala haraka - na uwezekano wa kushindwa kusaga baadhi ya vyakula na kukabiliwa na gesi, hutokea,” anasema Hill.



Post a Comment

0 Comments