Ticker

6/recent/ticker-posts

Suluhu ya Janga la Usugu wa vimelea dhidi ya dawa duniani yatafutwa



Suluhu ya Janga la Usugu wa vimelea dhidi ya dawa duniani yatafutwa

Usugu wa dawa hutokea pale ambapo vimelea vya magonjwa kama vile bakteria,virusi n.k vinapokuwa vimebadilika katika kipindi fulani na hivyo haviwezi tena kutibika kwa kutumia dawa zilizopo.

Viongozi wa dunia na wataalamu wa afya leo wamekusanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani wakitafta suluhu ya janga la usugu wa vimelea dhidi ya dawa, UVIDA au AMR kwa lugha ya kiingereza, na hatimaye kupitisha azimio la kisiasa la kukabiliana na tishio hilo la kiafya linalozidi kukua kila uchao.

Akizungumza na waandishi wahabari wakati wa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amegusia ukubwa wa suala hilo, akisema UVIDA au AMR husababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 1 kila mwaka.

“Azimio hili ni ishara thabiti kutoka kwa nchi kwamba wameazimia kutatua kitisho hiki cha kimataifa,” amesema Dkt. Tedros akiongeza kuwa “leo hii UVIDA ni moja ya vitisho vikubwa zaidi vya afya duniani. UVIDA inaweza kurudisha nyuma kwa miaka 100 maendeleo ya kiafya yaliyopatikana duniani, kwa kufanya maambukizi yanayoweza kutibika haraka, kuwa chanzo kikubwa cha Vifo.

Lengo la azimio ni kupunguza vifo kwa asilimia 10 ifikapo 2030

Pia amesisitiza kuwa hakuna taifa lililo na kinga dhidi ya kitisho hicho, ijapokuwa nchi za kipato cha chini na kati zinabeba mzigo mkubwa zaidi.

Ameeleza kwamba lengo la azimio hilo ni kupunguza vifo vihusianavyo na UVIDA kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Kufikia lengo hilo la kwenye azimio, kunahitaji kuchukua hatua sio kwenye sekta ya afya ya binadamu pekee, bali pia sekta ya afya ya wanyama na mazingira,” ametanabaisha.

Dkt. Tedros amesema kwamba WHO pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Afya na Chakula, FAO, afya ya Wanyama, WOAH, na lile la mazingira, UNEP yanashirikiana chini ya mpango mmoja wa AFYA MOJA ili kutatua suala hilo.

Wengi wetu hatumalizi dozi ya dawa - Mottley

Akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari ni Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley ambaye ameelezea UVIDA kama  janga linalokua kimya kimya.

Ametaja matumizi holela au matumizi ya kupita kiasi ya dawa za kuua vimelea vya magonjwa kuwa kichochea kikubwa cha usugu.

Mottley amesema wengi wetu tunapata dawa za kuua vimelea vya magonjwa Tunatumia kwa siku chache. Hatumalizi dozi kama tulivyoelekezwa na daktari.

Amesema “lazima tubadili tabia hii katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na hilo ndilo lengo la msingi kwanza kabisa, katika mkutano huu wa ngazi ya juu wa viongozi na azimio la kisiasa ili kuanza kuleta mabadiliko.”

“Hebu fikiria unapata maambukizi kwa kwenda bustanini au kujifungua mtoto au unapokwenda kwa daktari wa meno. Vitu hivi vinawea kumaliza maisha yako ndani ya saa 48 au 72 iwapo dawa mahsusi ya kuua vimelea vya magonjwa husika itashindwa kufanya kazi,” amesema Bi.Mottley.

UNEP, WOAH, FAO nao wazungumza

Kwa Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP, usugu huo hatari wa vimelea dhidi ya dawa unaweza kusababisha vifo vya watu milioni 40 na watu wengine milioni 160 kufa kwa magonjwa yahusianayo na UVIDA kati yam waka 2025 na 2050 iwapo hatua haitachukuliwa.

Mkurugenzi wa WOAH, Emmanuelle Soubeyran amekaribisha azimio hilo la kisiasa linalotilia mkazo kinga, hasa kwenye afya ya Wanyama na matumizi ya chanjo. Amesema chanjo zinaweza kusadia kuzuia magonjwa ambayo yanaweza kusababisha matumizi ya dawa za kuua vimelea mbali mbali.

Naye Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa FAO, Thanawat Tiensin, ametaka kuweko kwa hatua za pamoja ili kupunguza matumizi ya dawa za kuua vimelea kwenye sekta ya kilimo. “Na tunatarajia kuwa ifikapo mwaka 2030 tutaweza kupunguza matumizi duniani ya dawa za kuua vimelea kwenye mfumo mzima wa mazao ya kilimo na chakula, lakini tunahitaji msaada wenu.”



Post a Comment

0 Comments