Mtanzania wa Kwanza Agundulika na Maambukizi ya Homa ya Nyani (Mpox)
Mtanzania wa Kwanza Agundulika na Maambukizi ya Homa ya Nyani (Mpox)
WIZARA ya Afya imethibitisha kisa cha kwanza cha Mtanzania, kubainika amepata maambukizi ya homa ya nyani (Mpox). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Aidha, imesema Tanzania iko salama na hakuna mgonjwa wa Mpox aliyebainika hapa nchini hadi sasa.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Roida Andusamile, amesema Mtanzania huyo anayekadiriwa kuwa na miaka 32, alibainika kuwa na ugonjwa huo akiwa nchini Zambia.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma leo tarehe 11 Oktoba 2024, amesema taarifa ya kisa hicho waliipata jana kutoka mamlaka za serikali ya Zambia.
“Mtanzania huyu alivuka mpaka kutoka Tanzania kwenda Zambia mnamo tarehe 02 Septemba, 2024 kupitia mpaka wa Tunduma (Tanzania) na Nakonde (Zambia), akiwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Mpox,” amesema Roida.
Amesema mwezi mmoja baadaye yaani tarehe 02 Oktoba 2024, akiwa nchini humo, alikwenda katika kliniki mojawapo ambapo alipata matibabu ya awali na kuchukuliwa vipimo tarehe 04 Oktoba 2024, ambavyo vilithibitisha kuwa na maambukizi hayo.
“Tarehe 08 Oktoba 2024, vipimo vya maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ya Zambia vilithibitisha kuwa ni ugonjwa wa Mpox. Mgonjwa huyu bado anapata matibabu nchini Zambia…dalili za ugonjwa wa Mpox huweza kuonekana kati ya siku 3 hadi 21 tangu kuambukizwa. Hivyo, kwa kuwa Mtanzania huyu alianza kuonesha dalili mwezi mmoja baada ya kutoka nchini, ni dhahiri kuwa hakutoka nchini akiwa na maambukizi,” amefafanua.
Ameipongeza serikali ya Zambia kwa kubaini ugonjwa huo mapema, kumhudumia mgonjwa na kutoa taarifa kwa wakati.
Amesema Tanzania inaendelea kushirikiana na Zambia kufuatilia hali ya mgonjwa na kuhakikisha anapona na kurejea nchini, akiwa na afya njema.
“Wizara inapenda kuwahakikishia kuwa, bado Tanzania iko salama na hakuna mgonjwa wa Mpox aliyebainika hapa nchini hadi sasa. Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na itaendelea kutoa taarifa kwa umma.
“Wizara inatoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia kanuni za usafi, kutopeana mikono na kutoa taarifa kwa kutumia namba 199 ili kwa pamoja tuhakikishe ugonjwa huu hauingii nchini,” amesema Roida.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!