Wanne watajwa katika kinyang'anyiro cha kuwa Papa mpya

Wanne watajwa katika kinyang'anyiro cha kuwa Papa mpya

#1

Wanne watajwa katika kinyang'anyiro cha kuwa Papa mpya



Maelezo ya picha,Wanaotajwa kuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwa Papa (kushoto kwenda kulia) Kadinali Peter Kodwo Appiah Turkson, kadinali Pietro Parolin, kadinali Luis Antonio Gokim Tagle, na kadinali Fridolin Ambongo Besungu

Uamuzi wa nani atakayechaguliwa kuwa Papa ajaye unaweza kuwa na athari kubwa kwa Kanisa Katoliki na waumini wake wapatao bilioni 1.4 duniani kote. Lakini pia huu ni mchakato mgumu na usiotabirika kwa sababu nyingi.

Baraza la Makadinali litakutana kwa faragha ndani ya Kanisa la Sistine ili kujadili na kupiga kura hadi jina moja litakaposhinda.

Kwa kuwa asilimia 80 ya makardinali walipewa wadhifa na Papa Francis mwenyewe, hii itakuwa mara yao ya kwanza kumchagua papa, huku wakileta mtazamo mpana wa kimataifa.

Kwa mara ya kwanza katika historia, chini ya nusu ya Makadinali wapiga kura watakuwa kutoka Ulaya.

Na ingawa uteuzi huo ulifanywa na Papa Francis, haukuwa wa upande mmoja, yaani si wa mrengo wa "kizamani" pekee wala "wa kisasa" pekee.

Kwa hivyo, ni vigumu zaidi kutabiri nani atakayechaguliwa kuwa Papa ajaye.

Je, makardinali wanaweza kumchagua Papa kutoka Afrika au Asia? Au wataegemea mmoja wa watendaji waandamizi wa Vatican?

Haya hapa ni baadhi ya majina yanayotajwa kama warithi wa Francis, na majina mengine yanatarajiwa kujitokeza katika siku zijazo.

Pietro Parolin

Uraia: Muitalia

Umri: 70

Kardinali Parolin ni mtu wa maneno machache kutoka Italia, ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Jimbo la Vatican chini ya Papa Francis cheo kinachomfanya kuwa mshauri mkuu wa Papa.

Pia anasimamia Curia ya Roma, ambayo ni utawala mkuu wa Kanisa.

Kwa kuwa amewahi kufanya kazi kama "naibu papa", anaweza kuonekana kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa.

Wengine wanamwona kama mtu anayependelea diplomasia na mtazamo wa kidunia zaidi ya kushikilia misingi ya mafundisho ya Kanisa, jambo ambalo linaweza kuwa udhaifu kwa baadhi lakini nguvu kwa wengine.

Hata hivyo, amewahi kukosoa ndoa za jinsia moja, akisema kura ya mwaka 2015 iliyozipitisha nchini Ireland ilikuwa "pigo kwa ubinadamu".

Ingawa watabiri wanaweza kumpa nafasi, Parolin anafahamu methali maarufu ya Kiitaliano kuhusu uchaguzi wa papa: "Anayeingia kwenye uchaguzi akiwa tayari ni papa, atatoka akiwa tu kardinali."

Japokuwa Italia imetoa mapapa 213 kati ya 266 waliopita, haijatoa Papa kwa miaka 40 sasa, na mwelekeo wa Kanisa kuhamia nje ya Ulaya unaweza kuzuia Italia kutoa mwingine kwa sasa.

Luis Antonio Gokim Tagle*

Uraia: Mfilipino

Umri: Miaka 67

Je, Papa ajaye anaweza kutoka Asia?

Kadinali Tagle ana uzoefu mkubwa wa kiutume yaani amekuwa kiongozi wa Kanisa anayefanya kazi moja kwa moja na waumini badala ya kuwa mwanadiplomasia wa Vatican au mtaalamu wa sheria za Kanisa.

Kanisa Katoliki lina ushawishi mkubwa nchini Ufilipino, ambako takriban asilimia 80 ya watu ni Wakatoliki. Kwa sasa nchi hiyo ina Makadinali watano idadi ambayo inaweza kuwa na uzito ikiwa wote watamuunga mkono.

Yeye ni wa msimamo wa wastani, na amekuwa akifananishwa na Papa Francis kutokana na msisitizo wake juu ya masuala ya kijamii na huruma kwa wahamiaji.

Amesema wazi kupinga utoaji mimba, akilitaja kama "aina ya mauaji", jambo linaloendana na msimamo wa Kanisa kwamba uhai huanza wakati wa kutungwa kwa mimba.

Lakini mwaka 2015, alipokuwa Askofu Mkuu wa Manila, alitoa wito kwa Kanisa kufikiria upya ukali wake dhidi ya mashoga, waliotalikiana, na akina mama wasio na waume, akisema kuwa ukali huo umesababisha majeraha ya kudumu na kuacha watu wakihisi "wamewekwa alama".

Ameshawahi kutajwa kuwa kati ya wanaopewa nafasi ya kuwa Papa tangu mwaka 2013.

Alipoulizwa miaka 10 iliyopita kuhusu tetesi hizo, alijibu: "Nazichukulia kama utani! Zinachekesha."

Fridolin Ambongo Besungu*

Uraia: Mkongo

Umri: Miaka 65

Inawezekana kabisa Papa ajaye akatokea Afrika, ambako Kanisa linaendelea kushamiri.

Kadinali Ambongo ni mmoja wa wanaopewa nafasi, akiwa ametoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ameshika wadhifa wa Askofu Mkuu wa Kinshasa kwa miaka saba na aliteuliwa kuwa kadinali na Papa Francis.

Ni mkosoaji mkubwa wa ndoa za jinsia moja, akisema kuwa "muungano wa watu wa jinsia moja ni kinyume na maadili ya kitamaduni na ni uovu wa asili."

Ingawa Ukristo ni dini kubwa DRC, Wakristo nchini humo wamekumbana na mateso na vifo kutoka vita vya wenyewe kwq wenyewe. Katika mazingira hayo, Kadinali Ambongo anaonekana kama mtetezi imara wa Kanisa.

Lakini mwaka 2020, alieleza msimamo wa kuvumiliana kidini, akisema: "Wa-Protestanti wabaki wa-Protestanti, Waislamu wabaki Waislamu. Tutashirikiana nao, lakini kila mtu abaki na utambulisho wake."

Kauli kama hizo zinaweza kuwafanya baadhi ya makadinali kujiuliza kama anakubaliana kikamilifu na mtazamo wa Kanisa wa kueneza injili kote ulimwenguni.

Peter Kodwo Appiah Turkson*

Uraia: Mghana

Umri: Miaka 76

Kama atachaguliwa, Kardinali Turkson atakuwa Papa wa kwanza kutoka Afrika katika kipindi cha miaka 1,500.

Kama Ambongo, amewahi kusema hatamani nafasi hiyo. "Sina hakika kama kuna mtu anayetamani kuwa Papa," aliiambia BBC mwaka 2013.

Alipoulizwa kama Afrika ina nafasi nzuri ya kutoa Papa kutokana na ukuaji wa Kanisa barani humo, alisema uchaguzi wa Papa haupaswi kuzingatia takwimu tu, kwa sababu "vigezo hivyo huchanganya mwelekeo."

Yeye alikuwa Mghana wa kwanza kuteuliwa kuwa Kadinali, mwaka 2003 chini ya Papa Yohane Paulo II.

Ni mpiga gitaa aliyecheza kwenye bendi ya muziki wa funk, na anajulikana kwa ushwwishi wake wenye nguvu.

Kama Makadinali wengi kutoka Afrika walivyo, yeye pia ana misimamo ya kihafidhina.

Hata hivyo, amepinga sheria kali dhidi ya mashoga katika nchi kama Ghana.

Katika mahojiano ya 2023 na BBC, wakati Ghana ilikuwa inajadili muswada wa kuwahukumu watu wa LGBTQ+, Turkson alisema kuwa "ushoga haupaswi kuhesabiwa kama kosa."

Lakini mwaka 2012, aliwahi kukosolewa kwa kutoa kauli za kuchochea hofu kuhusu kuenea kwa Uislamu barani Ulaya katika kongamano la maaskofu Vatican, jambo ambalo baadaye aliomba msamaha.

Via:Bbc

Papa mpya anachaguliwa vipi?22 Aprili 2025

Hizi ndizo saa za mwisho za Papa zilivyokuwa22 Aprili 2025

Mfahamu Kadinali Kevin Farrell, anayeongoza Vatican baada ya kifo cha Papa22 Aprili 2025

Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu

Reply


image quote pre code