Amuua mwenza wake kwa kumshutumu kumuambukiza UKIMWI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, linamshikilia Samwel Emmanuel maarufu Nzaliya (20) mkazi wa kijiji cha Nata Wilaya ya Serengeti kwa tuhuma za mauaji ya Josephina Magani( 52).
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, amesema tukio limetokea Mei 7, 2025 majira ya saa saba usiku katika kitongoji cha Mamaswe Kijiji cha Nata, ambapo Emmanuel alimchoma Josephina kwa kutumia kitu chenye ncha kali maeneo ya tumboni na kusababisha kumwaga damu nyingi na kupelekea kufariki dunia.
“ Mtuhumiwa mara baada ya Kutenda kosa hilo aliuburuza mwili wa marehemu kutoka nyumbani kwake na kuutumbukiza kwenye shimo ambalo lilikuwa linatumika kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu” amesema Kamanda Lutumo.
Ameongeza kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio ni ugomvi baina ya marehemu na mtuhumiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mtuhumiwa alikuwa anamshtumu marehemu kumuambukiza maradhi ya ugonjwa wa ukimwi kwani walikuwa wakiishi kama mume na mke.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa kwa vyombo husika ili malalamiko yaweze kushughulikiwa kisheria.
Reply
image quote pre code