Breaking: Chukueni tahadhari dhidi ya uwepo wa COVID 19
Wizara ya Afya imesema imeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za kila siku kuhusu magonjwa ya mlipuko pamoja na tetesi za uwepo wa magonjwa hayo nchini ambapo imesema tangu February hadi April 2025, ufuatiliaji wa virusi vya Covid 19 umeonesha ongezeko la maambukizi kutoka 1.4% (Wagonjwa wawili kati ya Watu 139 waliopimwa) mwezi February hadi 16.3% (Wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) mwezi March, na kisha 16.8% (Wagonjwa 31 kati ya Watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025.
Taarifa iliyotolewa leo May 20,2025 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe imesema “Ugonjwa wa UVIKO-19, ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza nchini March 2020, umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama yalivyo magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa, hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huu imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huu mwaka 2020, kwa kipindi hiki ongezeko hili linaonekana zaidi katika Mkoa wa Dar es salaam, Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa nchini na kutoa taarifa”
“Katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2025, tumeshuhudia ongezeko la tetesi zinazohusiana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa katika jamii hapa nchini, hasa katika mkoa wa Dar es salaam, kwa kutumia mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, ambayo imekuwepo tangu mwaka 2008, tumekuwa tukifuatilia mwenendo wa magonjwa haya ili kubaini aina za vimelea vinavyosababisha maambukizi, ongezeko la visa, pamoja na uwezekano wa kujitokeza kwa kirusi kipya chenye uwezo wa kusambaa kwa haraka”
“Vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza hali ambayo imekuwa ikionekana pia katika miaka iliyopita na ndiyo maana hujulikana kama ‘Seasonal influenza”, vipimo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya kinachoweza kusambaa kwa haraka na kusababisha mlipuko wa aina ya Pandemiki” Cc:MillardAyoUPDATES