Mafuriko bwawa la nyumba ya Mungu yawakumba ngorika

Mafuriko bwawa la nyumba ya Mungu yawakumba ngorika

#1

Mafuriko bwawa la nyumba ya Mungu yawakumba ngorika

BAADHI ya wakazi wa Kata ya Ngorika wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kufurika kwa bwawa la Nyumba ya Mungu.

Diwani wa kata ya Ngorika Albert Msole amesema baadhi ya wakazi wa eneo hilo nyumba zao zimezungukwa na maji.

Msole amesema baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nyumba ya Mungu wanahitaji boti ili waweze kuvuka upande wa pili wa bwawa hilo ili wakapate huduma za kijami.

"Baadhi ya nyumba zimezingirwa na maji, msikiti umezungukwa na maji hivyo jamii kushikwa na sintofahamu kutokana na hali hiyo," amesema Msole.

Ameeleza kuwa chanzo cha mafuriko hayo ni kujaa kwa bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo linatumika kwa chanzo cha nishati ya umeme na kuvua samaki.

"Hii hali tuliizoea inatokea kila baada ya miaka mitano au 10 ila kutokana na mabadiliko ya tabia nchi huwa tunakumba na mafuriko haya kila baada ya mwaka," amesema Msole.

Ametoa ombi kwa halmashauri ya wilaya hiyo kununua mashine ya injini ya boti inayomilikiwa na Simanjiro ili isaidie watu kuvuka eneo moja kwenda lingine

"Pia tunaomba viongozi wa wilaya watembelee eneo hilo ili kujionea hali ilivyo n pia kuwapa pole waliokumbwa na adha hiyo," amesema Msole.

Mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo Julius John amesema baadhi ya wakazi wa Nyumba ya Mungu wamepata hasara ya mafuriko hayo.

"Wengine wanaishi kama wapo kwenye kisiwa kwani wanashindwa kutoka eneo moja kwenda sehemu nyingine kutokana na mafuriko hayo," amesema.

Diwani wa kata ya Msitu wa Tembo, Kaleya Mollel amesema japokuwa mafuriko yaliyosababishwa na kujaa kwa bwawa la Nyumba ya Mungu limefikia eneo hilo madhara yake siyo makubwa.

Mollel amesema ni athari ya mafuriko hayo kwa wakazi wa eneo lake siyo kubwa kama ilivyo kwenye kata ya Ngorika.

Hata hivyo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota ameeleza kuwa wanatarajia kununua boti mpya kwani iliyopo imechakaa.

"Hiyo boti iliyopo imechakaa hivyo inapaswa kununuliwa mpya kwani ukinunua mashine ya injili pekee tunaweza kusababisha madhara mengine," amesema Makota.




Reply


image quote pre code