Mchakato wa kumchagua Papa Mpya waanza leo, fahamu taratibu nzima

Mchakato wa kumchagua Papa Mpya waanza leo, fahamu taratibu nzima

#1

Mchakato wa kumchagua Papa Mpya waanza leo, fahamu taratibu nzima



Makadinali wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura wanakutana katika baraza la siri kuchagua Papa mpya.

Mkutano huo wa siri unafanyika katika kanisa dogo la Sistina, Mei 7 ukijumuisha makadinali 135 kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Mkutano huu unafuatia kifo cha Papa Francis, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88 siku ya Jumatatu ya Pasaka 21 April, na mazishi yake kufanyika siku ya Jumamosi 26 April.

Hakuna muda maalum uliowekwa kumchagua Papa mpya, lakini mikutano miwili ya awali ya uchaguzi wa Papa iliyofanyika mwaka 2005 na 2013, ilidumu kwa siku mbili tu.

Nani anayeweza kupiga kura?

Kwa zaidi ya miaka 750, sheria kali zimetawala orodha ya makadinali wanaokusanyika kumchagua papa. Na kumekuwa na usiri mkubwa wa kuzuia taarifa kutoka nje kuingia ndani na za ndani kutoka nje. Makadinali wakisalia na utumishi zaidi kwenye kuchagua kuliko ushawishi wowote. Kwenye kulinda usiri hata baadhi ya vyakula vinazuiwa kuingizwa ndani. Kwa mfano kuku ni kitu ambacho kimepigwa marufuku kutoka kwenye meza ya makadinali kwa karne nyingi, kwani vinaweza kutumika kupitisha ujumbe wa siri.

Kuna makadinali 252 kote ulimwenguni kufikia tarehe 19 Februari 2025, ambao kwa kawaida pia ni maaskofu. Na wale walio chini ya umri wa miaka 80 ndio wanaostahili kumpigia kura papa mpya.

Idadi ya "makadinali wanaopiga kura" kwa kawaida hupunguzwa hadi 120, lakini kwa sasa kuna makadinali 135 kati yao ambao wana vigezo vya kushiriki katika kumchagua Papa mpya. (Papa Francis aliteua Makadinali wapya 21 mwezi Desemba 2024.)

Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya makardinali wenye umri wa kupiga kura katika historia ya Kanisa Katoliki.

Makardinali ni washiriki wakuu wa makasisi wa Kanisa Katoliki na kwa kawaida huwekwa wakfu kuwa maaskofu.

Papa Francis aliteua idadi kubwa ya makardinali wenye umri wa kupiga kura, 108, wakati wengine walichaguliwa na watangulizi wake Papa Benedict XVI na Mtakatifu John Paul II.

Utaratibu wa uchaguzi wa Papa

Katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, wanafanya Misa (ibada la Kikristo) katika Kanisa la St Peter's Basilica. Kisha wanakusanyika katika Kanisa la Sistine la Vatikani. Huko, agizo la "extra omnes" hutolewa. Ni lugha ya Kilatini ikiwa na maana "kila mmoja atoke nje."

Kuanzia wakati huo, Makadinali wote watawekwa ndani ya Vatican hadi papa mpya atakapochaguliwa.

Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni, alisema kwamba makardinali watashiriki katika misa takatifu katika Basilika ya Mtakatifu Petro, baada ya hapo wale wanaostahili kupiga kura watakusanyika katika Kanisa la Sistine kwa ajili ya upigaji kura wa siri.

Mara tu wanapoingia katika Kanisa la Sistine, makardinali hawapaswi kuwa na mawasiliano yoyote na ulimwengu wa nje hadi Papa mpya atakapochaguliwa.

Kuanzia siku ya pili na kuendelea, hupiga kura mara mbili kila asubuhi, na mara mbili kila alasiri, hadi mgombeaji wa Upapa apatikane mmoja.

Jinsi kura inavyopigwa

Katika zoezi la kura, kila Kadinali anaye piga kura huandika jina la mgombea anayempendelea kwenye karatasi za kupigia kura. Kila kardinali hupiga kura yake kwenye karatasi rahisi iliyoandikwa kwa Kilatini: "I elect ...as Supreme Pontiff" (Ninachagua.... kuwa Papa Mkuu), na huongeza jina la mgombea wanayemchagua.

Kila kardinali anaandika chaguo lake kwenye kura na kuiweka kwenye chupa kubwa la fedha na dhahabu.

Ili kuficha kura, Makadinali wanaambiwa wasitumie mtindo wao wa kawaida wa mwandiko.

Mshindi anahitaji theluthi mbili ya wingi ili kuchaguliwa.

Iwapo mkutano wa uchaguzi (conclave) utamaliza siku ya tatu bila kufikia uamuzi, makardinali wanaweza kusitisha zoezi kwa siku moja kwa ajili ya sala.

Kuna duru moja tu ya kupiga kura katika alasiri ya kwanza ya kikao hicho, lakini baada ya hapo makardinali watapiga kura hadi mara nne kila siku.

Ili kuchaguliwa kuwa Papa mpya, mgombea anahitaji kupata theluthi mbili ya kura zote – jambo ambalo linaweza kuchukua muda.

Baada ya kuchaguliwa nini hufuata?

Mara baada ya Papa kushinda kura, papa mpya anaulizwa: "Je, unakubali kuchaguliwa kwako kama Papa Mkuu?"

Anachagua jina ambalo anataka litumiwe kuitwa kama Papa. Kisha Makadinali wanampa heshima na kuahidi utii wao.

Wakati haya yote yanafanyika, Wakatoliki husubiri katika Uwanja wa St Peter's ulio karibu, wakitazama moshi ufuke kutoka kwenye bomba la Sistine Chapel.

Tangazo linatolewa kwenye roshani ya jengo la St Peter's Basilica kwa umati uliopo chini. Tangazo hilo husema, "habemus papam", ikiwa na maana: "Tumepata Papa."

Jina la Papa mpya linafichuliwa, na Papa mwenyewe anaonekana. Anatoa kauli fupi na kutoa baraka za "urbi et orbi" – ikiwa na maana kwa "mji na ulimwengu."

Baadaye, matokeo ya kila duru ya upigaji kura katika mkutano huo hupelekwa kwa Papa. Kisha hutiwa muhuri na kuwekwa katika hifadhi ya kumbukumbu ya Vatikani, na yanaweza kufunguliwa tu kwa amri ya Papa.

Kongamano refu zaidi katika historia ya kumchagua Papa lilidumu miaka miwili na miezi tisa, kuanzia 1268 - lakini katika siku za hivi karibuni mchakato wa kumchangua Papa umekuwa wa haraka zaidi, kwa wastani wa siku tatu tangu mwanzoni mwa Karne ya 20.

Papa Francis na mtangulizi wake Papa Benedict XVI walichaguliwa katika kipindi cha siku mbili tu.

Via:Bbc

Reply


image quote pre code