Hai. Mary Mushi (26), mkazi wa Kijiji cha Mungushi, Hai mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kuwaua wanawe wawili, mmoja wa miaka minne na mwingine wa miezi sita, kisha kujijeruhi, chanzo kikitajwa ni mgogoro wa kifamilia.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema limetokea leo Juni 20, 2025.
"Ni kweli tukio limetokea, mama anadaiwa kuwaua watoto wake wawili na kisha yeye kujijeruhi kifuani, tumboni na kwenye koromeo kwa kitu chenye ncha kali," amesema Kamanda Mtagwa.
Kamanda Mtagwa amesema mwanamke huyo sasa yupo chini ya ulinzi na anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, mjomba wa watoto hao, Emmanuel Shija, amesema alifika eneo la tukio baada ya kupata taarifa na kukuta miili ya watoto hao tayari imeondolewa.
"Hii taarifa nimeipata baada ya kupigiwa simu na baba mkwe wake na mdogo wangu kwamba kuna mauaji yametokea, wajomba zangu wawili, Glory na mdogo wake wameuawa," amesema mjomba wa watoto hao.
“Baada ya kuona miili imeondolewa, nilienda Hospitali ya Wilaya ya Hai, nikakuta mjomba wangu wa kwanza na wa pili. Nimeshtuka sana na kushindwa kuelewa chanzo cha tukio hili, lakini kweli nimeumia sana kutokana na kilichotokea,” amesema.
Amesema mama wa watoto hao yupo hospitalini KCMC akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kujijeruhi sehemu kubwa ya mwili wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mungushi, Lameck Simon amesema tukio hilo limetokea leo mchana Juni 20, 2025 na alipokea taarifa hiyo kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji chake.
"Leo saa 6:30 mchana eneo la Mungushi mama amewaua watoto wake wawili kwa kuwachoma visu hadi kufa na yeye mwenyewe akajichoma kisu na bahati nzuri aliwahiwa na kupelekwa hospitali," amedai mwenyekiti huyo.
Aidha, amesema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina.
Miili ya watoto hao sasa imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa ajili ya taratibu za uchunguzi.
Hii ni tukio la tatu ndani ya takriban wiki moja baada ya matukio mawili kutokea mkoani Tabora, ambapo mama mwenye umri wa miaka 25 anadaiwa kujitoa uhai pamoja na watoto wake wanne kwa kunywa sumu ya kuulia wadudu.
Tukio la kwanza lilitokea Juni 15, 2025, katika Kata ya Kalunde, Manispaa ya Tabora, ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 21 anadaiwa kujiua kwa njia hiyo.
Akizungumzia tukio mama kudaiwa kuwaua watoto wake wanne kwa kinachodaiwa wivu wa mapenzi lilitokea katika Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alimtaja mama aliyefariki kuwa ni Kang'wa Mahigi, mkazi wa Kata ya Lugubu, Wilaya ya Igunga.
Kwa mujibu wa Abwao chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi ambapo Mahigi (25) alikuwa ni mke mkubwa.
Abwao aliwataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Sengi James (8), Simon James (6), Elisha James (3), na Kashinje James (miezi saba), pamoja na mama yao, Kang'wa Mahigi (25), ambaye ndiye anadaiwa kutekeleza mauaji hayo.
REPLY HAPA
image quote pre code