DAR ES SALAAM;RAIS Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kufuatia ajali iliyotokea jana Same mkoani Kilimanjaro, huku akiwataka madereva waendelee kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria za usalama barabarani.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya ndugu zetu 37 na majeruhi 30 kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea jana jioni eneo la Sabasaba, Barabara Kuu ya Moshi - Tanga, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kwa magari mawili kugongana na kuungua moto.
"Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka. Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, familia zote za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi Mungu awape faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.
“Kama ambavyo nilieleza Juni 27 katika hotuba yangu ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ajali za barabarani zimeendelea kugharimu maisha ya wapendwa wetu. Ninawasisitiza madereva kuendelea kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria za usalama barabarani, na Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kikamilifu sheria hizo," ameandika Rais Samia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.
REPLY HAPA
image quote pre code