Aliyekuwa kocha mkuu wa Klabu ya Yanga ya Tanzania, Miloud Hamdi (54), raia wa Algeria, ameteuliwa rasmi kuwa kocha mkuu wa Klabu ya Ismaily SC ya Misri kwa mkataba wa mwaka mmoja, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi endapo pande zote zitakubaliana.
Hamdi anajiunga na Ismaily akitokea Yanga , ambako aliandika historia ya kipekee kwa kuiwezesha klabu hiyo kutwaa mataji matatu makubwa katika msimu wa 2024/2025. Chini ya uongozi wake, Yanga ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB (FA Cup), na Kombe la Muungano.
Kuteuliwa kwa Hamdi kunakuja wakati Ismaily SC ikisaka kurejesha heshima yake katika soka la Misri, ikiwa ni mojawapo ya vilabu vyenye historia ndefu na mafanikio ya muda mrefu katika bara la Afrika.
Hatua hiyo pia inaashiria mwanzo mpya kwa Yanga , ambayo sasa italazimika kusaka kocha mpya atakayeendeleza mafanikio na ramani ya ushindani kimataifa ambayo Hamdi ameijenga.
Kocha huyo mwenye uzoefu, ambaye amewahi pia kuzinoa klabu kadhaa barani Afrika na Asia, anatarajiwa kuanza kazi mara moja akiungana na kikosi cha Ismaily kujiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Misri.
REPLY HAPA
image quote pre code