kumeibuka mjadala mkubwa kuhusu kutokuwepo kwa Cristiano Ronaldo kwenye mazishi ya Mchezaji mwenzake wa Timu ya Taifa ya Ureno, Diogo Jota, aliyefariki Dunia pamoja na kaka yake, André Silva, katika ajali ya Gari huko Zamora, Hispania, Julai 3, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Gazeti la Record la Ureno, Ronaldo aliamua kutohudhuria mazishi hayo kutokana na maumivu ya kihisia aliyoyapata baada ya kumpoteza Baba yake, José Dinis Aveiro, mwaka 2005. Tukio hilo lilimuathiri sana, na tangu wakati huo amekuwa akiepuka kuhudhuria hafla za mazishi za Watu wa karibu ili kuepuka kurejea katika hali hiyo ya huzuni.
Gazeti la Mirror Football liliripoti kuwa CR7 alihofia uwepo wake ungeweza kuvuruga utaratibu wa mazishi hayo kutokana na mvuto wake mkubwa kwa vyombo vya habari na Mashabiki. Aliona kuwa ni vyema kutoa nafasi kwa familia ya Jota kuomboleza kwa utulivu na faragha. Ingawa hakuwepo kimwili, Ronaldo alitoa pole zake kwa familia ya Jota kupitia mitandao ya kijamii, akieleza:
"Haieleweki. Tulikuwa pamoja hivi karibuni katika Timu ya Taifa, na ulikuwa umeoa tu. Kwa familia yako, Mkeo na Watoto wako, natuma rambirambi zangu na kuwatakia nguvu zote za Dunia. Najua utakuwa nao daima. Pumzikeni kwa amani, Diogo na André. Tutawakumbuka daima."
Pia, Ronaldo aliahidi kuwa karibu na familia ya Jota na kuwasaidia kadri watakavyohitaji katika kipindi hiki kigumu.
Kutokuwepo kwa Ronaldo kwenye mazishi hayo kuliibua hisia mseto miongoni mwa Mashabiki na vyombo vya habari. Baadhi walielewa uamuzi wake, wakizingatia sababu alizotoa, huku wengine wakieleza masikitiko yao kwa kutomwona Nahodha wa Timu ya Taifa akitoa heshima za mwisho kwa Mchezaji mwenzake.
Uamuzi wa Cristiano Ronaldo kutohudhuria mazishi ya Diogo Jota ulitokana na sababu za kihisia na nia ya kutoa nafasi kwa familia ya Marehemu kuomboleza kwa utulivu. Licha ya kutokuwepo kimwili, Ronaldo alionesha mshikamano na familia ya Jota kwa njia nyingine, ikiwa ni pamoja na kutoa pole zake na kuahidi msaada kwa familia hiyo.
REPLY HAPA
image quote pre code