Ugonjwa wa Kipindupindu watesa Afrika Magharibi na Kati – DRC ikiwa Kitovu cha Mlipuko
Wakati mvua zikiripotiwa kuanza kunyesha katika maeneo mbalimba ya Afrika Magharibi na Kati, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Watoto UNICEF limeripoti kuwa takribani watoto 80,000 wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu.
Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo kutoka Dakar Senegal imeripoti kuwa nchi 12 zimeathirika na mlipuko huu unaoenea kwa kasi, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo -DRC ikitajwa kuwa ndiyo iliyoathirika zaidi.
DRC hali ni mbaya
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya ya DRC, zaidi ya wagonjwa 38,000 wa kipindupindu na vifo 951 vimeripotiwa nchini humo mwezi huu wa Julai pekee. Takribani asilimia 25.6 ya wagonjwa wa kipindupindu ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Afrika Magharibi na Kati, Gilles Fagninou amesema “Hii ni hali ya dharura inayohitaji hatua za haraka, ni suala la maisha na kifo.”
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na majimbo ya South Kivu, North Kivu, Haut Katanga, Tshopo, Haut Lomami, Tanganyika, na Maniema.
Jiji la Kinshasa limeingia kwenye hali ya dharura baada ya ongezeko kubwa la maambukizi ndani ya wiki nne zilizopita kufuatia mafuriko makubwa na mvua zinazoendelea, huku kiwango cha vifo kwa wagonjwa kikifikia asilimia 8, hiki ni kiwango cha kutisha kwa muktadha wa ugonjwa huu unaotibika haraka iwapo utagundulika mapema.
“Hali mbaya ya mvua, mafuriko na watu wengi waliolazimika kuhama makazi yao vinaongeza kasi ya kusambaa kwa kipindupindu na kuweka maisha ya watoto hatarini,” amesemaFagninou
UNICEF inaonya kuwa bila hatua madhubuti za kudhibiti mlipuko huu, DRC inaweza kukumbwa na janga la kipindupindu kubwa zaidi tangu mwaka 2017.
Hali ilivyo katika mataifa mengine
Nchi nyingine zilizoathirika ni Nigeria (wagonjwa 3,109 na vifo 86), Chad (wagonjwa 55 na vifo 4), Ghana (wagonjwa 612), Côte d’Ivoire (wagonjwa 322 na vifo 15), na Togo (wagonjwa 209 na vifo 5).
Nchi kama Niger, Benin, Liberia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Cameroon zinaendelea kufuatiliwa kwa karibu.
Mkuu huyo wa kanda wa UNICEF amesema “Tupo kwenye mbio dhidi ya wakati, tukishirikiana na serikali kutoa huduma muhimu kama maji safi na salama, lishe na huduma za afya kwa watoto walio katika hatari kubwa. Tunafanya kila jitihada kuhakikisha hakuna mtoto anayesahaulika.”
UNICEF imekuwa mstari wa mbele kusambaza huduma za afya, maji safi, vifaa vya usafi na katika utoaji wa chanjo, pamoja na kuelimisha jamii kuhusu kinga na tiba ya kipindupindu.
Hata hivyo, shirika hilo linahitaji dola milioni 20 ndani ya miezi mitatu ijayo ili kuongeza kasi ya msaada katika nchi zilizoathirika.
image quote pre code