Wakati asilimia 91 ya watu wazima wa DRC wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, (VVU) wanapokea matibabu, ni asilimia 44 tu ya watoto wanaopata huduma hiyo – pengo lisilokubalika ambalo limekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeazimia kulitatua.
Katika hatua ya aina yake ya kuziba pengo la muda mrefu katika matibabu dhidi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU, Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amezindua mpango wa kitaifa wa kutokomeza maambukizi ya UKIMWI kwa watoto nchini humo ifikapo mwaka 2030.
"Nchi yetu haiwezi tena kuvumilia watoto kuzaliwa na kukua na VVU wakati kuna zana za kuzuia, kugundua, na kutibu maambukizi haya kwa ufanisi," amesema Rais Tshisekedi wakati wa uzinduzi uliofanyika kwenye mkutano wa magavana huko Kolwezi, jimboni Lualaba.
"Kutokomeza UKIMWI kwa watoto ni wajibu wa maadili, hitaji la haki ya kijamii, na kiashiria cha heshima ya kibinadamu," ameongeza Rais Tshisekedi, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na UKIMWI, UNAIDS.
UNAIDS inasema mpango huu mpya, unaoitwa IPESE (Initiative Présidentielle pour l’Élimination du Sida chez l’Enfant), ni ishara ya kujitolea upya kitaifa kuwafikia watoto ambao, licha ya mafanikio makubwa katika huduma za VVU kwa watu wazima, bado wameachwa nyuma kwa kiasi kikubwa.
Nchini DRC, maelfu ya watoto bado wanaambukizwa VVU kila mwaka kutokana na ukosefu wa upimaji kwa wanawake wajawazito, fursa iliyopotea ya kuokoa maisha ya akina mama na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Vipaumbele 4 muhimu
Mpango huu wa miaka mitano kutoka kwa Rais — ukiungwa mkono na ufadhili wa awali wa dola milioni 18 kutoka serikali ya kitaifa — unalenga kutoa mwitikio wa pamoja na wa kimkakati kupitia uongozi madhubuti wa kisiasa katika ngazi zote, ikiwemo magavana wa mikoa.
DRC imejizatiti kuharakisha maendeleo katika maeneo manne ya kipaumbele:
Kuboresha uchunguzi wa mapema na matibabu kwa watoto, vijana, na wanawake wajawazito
Kuzuia maambukizi mapya miongoni mwa watoto, vijana, na akina mama
Kuhakikisha matibabu ya haraka na ya moja kwa moja kwa wote waliogundulika kuwa na maambukizi
Kuondoa vikwazo vya kimfumo vinavyowazuia vijana kupata huduma za afya, kupitia njia zenye heshima, ushirikishwaji, na urafiki kwa vijana
Watoto wanaachwa nyuma
Wakati asilimia 91 ya watu wazima wanaoishi na VVU nchini DRC sasa wanapata matibabu ya kupunguza makali ya virusi (ARV), ni asilimia 44 tu ya watoto wanaoishi na VVU wanaopata huduma hizo — pengo ambalo limekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Shukrani kwa ushirikiano kati ya serikali, jamii za kiraia, jumuiya za wenyeji, na washirika wa kimataifa kama PEPFAR, Mfuko wa Dunia, (Global Fund), UNAIDS, na Taasisi ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation, ufanisi wa matibabu kwa watu wazima umeongezeka kwa kasi. Lakini kwa watoto, mfumo bado unasuasua.
Kila mwaka, maelfu ya watoto wa DRC wanaambukizwa VVU, mara nyingi kwa sababu wanawake wajawazito hawachunguzwi — fursa iliyopotea ya kuokoa maisha ya mama na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Hali hii inaonesha matatizo ya kimfumo: upatikanaji duni wa huduma bora za afya ya uzazi na jinsia kwa wanawake, ukosefu wa ujumuishaji mzuri wa huduma za VVU katika huduma ya afya ya mama na mtoto, minyororo dhaifu ya usambazaji wa dawa, na uratibu hafifu kati ya huduma za umma na jamii.
Huko Kolwezi, jimboni Lualaba nchini DRC, Rais Tshisekedi amesema kwamba DRC haitavumilia tena "watoto kuzaliwa na kukua wakiwa na VVU, ilhali kuna vifaa vya kuzuia, kugundua na kutibu maambukizi haya kwa ufanisi."
Tumaini jipya
UNAIDS imekaribisha mpango huu kama hatua muhimu inayohitajika sana wakati huu ambapo rasilimali za maendeleo ziko kwenye shinikizo kubwa.
"Katika kipindi ambapo ufadhili wa maendeleo unakabiliwa na changamoto na mifumo ya kusaidia walio hatarini zaidi imebanwa, uongozi wa Rais Félix Tshisekedi ni taa ya matumaini," amesema Dkt. Susan Kasedde, Mkurugenzi wa UNAIDS nchini DRC. “UNAIDS inaunga mkono kikamilifu mpango huu jasiri na wa kuhamasisha.”
Kupitia mpango huu, DRC inalenga kubadili mwelekeo wa kizazi kizima cha watoto ambao kwa muda mrefu wameachwa nyuma katika mapambano dhidi ya VVU.
"Tunatangaza ahadi ya kitaifa kuhakikisha kila mtoto wa Kongo ana haki ya kuzaliwa na kukua bila mzigo wa VVU," amesema Rais Tshisekedi. “Tuna njia za kufanikisha hili — na juu ya yote, tuna wajibu.”
TAGS: Afya/Afrika/DRC/VVU/PEPFAR/UNAIDS
REPLY HAPA
image quote pre code