Madaktari wa Uingereza wamebuni njia mpya ya kusafisha utumbo kukabiliana na vijidudu sugu vinavyojulikana kama "superbugs," wakitumia vidonge vyenye kinyesi kilichokaushwa na kugandishwa.
Utafiti huu mpya unalenga wagonjwa ambao wameambukizwa bakteria sugu ndani ya miezi sita iliyopita.
Katika vipimo hivi, kinyesi kinachukuliwa kutoka kwa wachangiaji wenye afya. Kila sampuli ya kinyesi hupimwa ili kuhakikisha haina bakteria hatari, chakula ambacho hakijameng'enywa huondolewa, kisha kinakaushwa kwa kugandishwa na kusagwa kuwa unga.
Unga huo huhifadhiwa kwenye tembe (kidonge) inayoweza kupita tumboni bila kuathirika na kufika kwenye utumbo. Huko, inafunguka na kutoa unga huo kwenye kinyesi.
Huu ni mpango mpya wa kupambana na vijidudu sugu dhidi ya antibiotics na ambavyo huua karibu watu milioni moja kila mwaka.
Kwa mujibu wa Dkt. Blair Merrick, anayeongoza utafiti wa vidonge hivi,anasema utumbo ni "chanzo kikubwa zaidi cha usugu wa viua sumu katika mwili wa binadamu." Vijidudu sugu dhidi ya dawa vinaweza kuenea kutoka kwenye utumbo kwenda sehemu nyingine za mwili, kama vile njia ya mkojo au damu, na kusababisha maambukizi.
Wazo la kidonge cha kinyesi si jipya. Upandikizaji wa kinyesi (kuingiza kinyesi kilichosindikwa chenye vijidudu vyenye manufaa kwenye utumbo) hutumika kutibu kuhara kunakosababishwa na bakteria aina ya Clostridium difficile. Tiba hii iliwafanya wanasayansi kugundua kuwa kutumia vijidudu vyenye manufaa kunaweza pia kusaidia kutoa vijidudu vingine hatari kutoka kwenye utumbo na kusafisha utumbo.
Jaribio lilifanyika kwa wagonjwa 41 katika hospitali mbili za London, Uingereza ili kufungua njia kwa utafiti mkubwa zaidi.
REPLY HAPA
image quote pre code