Ikiwa ugonjwa hauambukizi, kunyonyesha ni salama
Grace Mhando, Mtaalamu wa lishe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili nchini Tanzania.
Zipo dhana na imani potofu mbalimbali kuusu unyonyeshaji maziwa kwa mtoto. Lakini pia iko hofu miongoni mwa jamii kuhusu mama mwenye changamoto za kiafya umnyonyesha mtoto wake iwe kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia ya chupa.
Ingawa Wiki ya Kimataifa ya Unyonyeshaji maziwa ya mama inayoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, imefika tamati Agosti 7, lakini elimu kuhusu suala hili muhimu kwa ustawi wa binadamu ni elimu endelevu kwani kila wakati mahali fulani duniani anapatikana mama mpya.
Selina Sylivester, Afisa Muuguzi anayewapokea wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika hospitali yenye historia ya zaidi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, Hospitali ya Taifa Muhimbili anaeleza kuhusu baadhi ya imani potofu wanazokutana nazo kuhusu unyonyeshaji.
“Unakutana na akina mama ambao wananyonyesha lakini wanakuwa na imani zao kutoka walikotoka kwamba mimi siwezi kunyonyesha mtoto au kukamua maziwa kumnywesha mtoto kwasababu niña ugonjwa labda kama Kisukari, Shinikizo la Damu, kwa hiyo anaamini kwamba akimnyinyesha mtoto akiwa na magonjwa kama hayo ataumia zaidi au kama ni shinikizo la damu itaongezeka badala ya kukaa katika hali ya kawaida.”
Madhali ugonjwa hauambukizi, kunyonyesha ni salama
Afisa Muuguzi, Selina Sylivester anaeleza kwamba wanawaondoa wasiwasi akina mama hao kuwa hata ukiwa na hali hizo za magonjwa sugu kama kisukari na shinikizo la damu unanyonyesha kama kawaida.
Rachel Chalo kabla ya kujifungua aligundulika kuwa ana ugonjwa wa Kisukari, shinikizo la damu na pumu. Mama huyu ambaye amepata mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati lakini anaendelea vizuri sana anathibitisha yaliyosemwa na Afisa Muuguzi hapo awali kuwa licha ya changamoto za kiafya za mama kuangaliwa kwa ukaribu, lakini pia kipaumbele kinaelekezwa katika kuhakikisha mtoto ananyonya maziwa ya mama angalau miezi sita ya mwanzo.
Maziwa ya ng’ombe je?
Lakini kuna sababu gani hasa ya kuhangaika hivi ikiwa pia kuna maziwa ya wanyama kama ng’ombe? Grace Mhando ni mmoja wa Maafisa Lishe wa wa Hospitali ya Muhimbili analifafanua hili kitaalamu akisema, “maziwa ya mama ni bora zaidi kuliko maziwa ya ng’ombe kwasababu maziwa ya mama yana virutubisho vya kinga vinavyomkinga mtoto dhidi ya magonjwa.” Mtaalamu huyo wa lishe anaeleza zaidi kuwa pia maziwa ya mama yana maji ambayo yanatosha kumfanya mtoto asihitaji kupewa maji ya kawaida.
Vipi kuhusu lishe ya mama mwenyewe? Afisa Lishe Grace Mhando anatoa ushauri kwamba mama mnyonyeshaji inabidi ale vyakula mbalimbali ambavyo ni salama na muhimu katika mwili, anywe maji ya kutosha, kufanya mazoezi na kupumzika vya kutosha ili kuufanya ubongo ufanye kazi yake vizuri kuzalisha maziwa ya kutosha.
image quote pre code