Je, Choo cha kukalia huweza kusababisha magonjwa?
Unapoingia kwenye choo cha kukalia kinachotumiwa na mamia ya watu wengine, unaweza kuwa unajiuliza; vimelea vya magonjwa huishi kwa muda gani kwenye choo hicho? Utapata magonjwa kwa kukaa na kujisaidia?
"Kinadharia, ndiyo [unaweza kupata magonjwa kupitia choo cha kukalia], lakini hatari hiyo iko chini sana," anasema Jill Roberts, profesa wa afya ya umma na vijidudu katika Chuo Kikuu cha Florida, Marekani.
Mfano magonjwa ya zinaa (STDs). Wengi wa bakteria na virusi vinavyoweza kusababishia magonjwa hayo, kuanzia kisonono hadi klamidia, hawawezi kuishi kwa muda mrefu nje ya mwili wa kiumbe, achilia mbali kwenye sehemu yenye baridi, ngumu kama juu ya choo cha kukalia.
Ndiyo maana mengi ya magonjwa ya zinaa huambukizwa tu kupitia mguso wa moja kwa moja wa sehemu za siri na kubadilishana maji maji ya mwili.
Ili kuwa hatarini, labda itokee bahati mbaya ya mtu kuhamisha majimaji ya mwili ya mtu mwingine kutoka kwenye choo cha kukalia hadi kwenye sehemu ya siri kupitia mkono au karatasi ya choo, anasema Roberts.
Ingawa ni vyema kuwa waangalifu na kudumisha usafi, kama vile kuepuka vyoo vichafu, lakini si jambo ambalo linapaswa kukukosesha usingizi.
“Kama ingekuwa rahisi kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kupitia vyoo vya kukalia, tungeona maambukizi ya mara kwa mara kwa watu wa rika zote, hata ambao hawana historia ya kufanya ngono," anasema Roberts.
Vile vile, Roberts anaongeza, hakuna uwezekano wa kupata ugonjwa unaoambukizwa kwa damu kupitia choo cha kukalia, hata kama utaikuta damu chooni. Damu hiyo haiwezi kusambaza vimelea vya magonjwa kwa urahisi bila kufanya ngono au kudungwa sindano chafu, anasema.
Pia ni vigumu kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo yaani UTI kupitia choo cha kukalia, anasema Roberts. Utapata UTI ikiwa tu utahamisha kinyesi kutoka kwenye choo cha kukalia hadi kwenye njia ya mkojo, lakini ni kiasi kikubwa cha kinyesi kitahitajika kwa maambukizi kutokea, anafafanua Roberts.
Ni rahisi zaidi kupata UTI kwa kufuta kinyesi chako karibu sana na sehemu zako za siri kuliko kukaa juu ya choo, anaongeza.
image quote pre code