Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na masuala ya wanawake Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Lilian Mnabwiru, amesema kuna vipindi vitatu anavipitia mwanamke anapofikia kikomo cha hedhi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Dailynews Digital, Dk Lilian ambaye pia ni mbobezi katika masuala ya upandikizaji mimba, amesema asilimia kubwa ya wanawake hukoma hedhi wakiwa na umri wa miaka 50 hadi 51.
“Kukoma kwa hedhi ni hali ya kawaida kwa mwanamke kulingana na vipindi vya maisha ukomo wa hedhi unaweza kutokea kwa wakati wowote, hali hii inatokea wakati miezi 12 mfululizo mwanamke hajaona siku zake au kwa lugha ninyingine kukosa hedhi kwa miezi hiyo mfululizo atakuwa amekoma,”ameeleza.
Dk Liliana anabainisha kuwa mara nyingi hali hiyo hutokea kuanzia miaka 40 mpaka 45 na kuna wanawake wanawahi kabisa miaka 35 na baadhi wanachelewa hadi umri wa miaka 60 mpaka 65.
Amebainisha kuwa kipindi kabla ya kuelekea kukoma hedhi kulingana na umri, imegawanyika katika vipindi, vitatu ambapo kipindi cha kwanza ni cha mpito kinachoanza na kuwa na mabadiliko, ambapo kichocheo kinaanza kushuka kwa kupunguza kasi na uwezo wa mayai kufanya kazi.
“Baada ya kipindi hicho inaweza kuchukua miaka nane ndipo anakoma hedhi moja kwa moja. Katika kapindi hicho baadhi ya mabadiliko atakayoona kwenye hedhi ni mwezi mmoja anaona mara mbili au tatu wengine zinapungua siku kama 20 wengine zinaongezeka siku 30,” amesema.
Imeandaliwa na Aveline Kitomary.
image quote pre code