Serikali yaamua kuhudumia familia za waliopotea kwenye machimbo Shinyanga

Serikali yaamua kuhudumia familia za waliopotea kwenye machimbo Shinyanga

#1

Serikali yaamua kuhudumia familia za waliopotea kwenye machimbo Shinyanga



Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza na familia ambazo zinasubili ndugu zao kuokolewa ajali ya Mgodi katika Machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga.

Serikali mkoani Shinyanga imeanza kuweka utaratibu wa kuzihudumia familia 18 ambazo ndugu zao wamefukiwa kwenye machimbo ya dhahabu ya Nyandolwa, wilayani Shinyanga, wakati jitihada za uokoaji zikiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alibainisha hayo Agosti 18, 2025, alipowasili eneo la tukio kushuhudia hali ya uokoaji na kuzungumza na familia zinazongoja ndugu zao kuokolewa.

Alisema kati ya watu 25 waliokuwa wamefukiwa na kifusi baada ya machimbo hayo kuporomoka Agosti 11, saba tayari wametolewa, wakiwemo watatu waliopatikana wakiwa hai na wanne waliopoteza maisha. Miili ya marehemu hao imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Mhita alieleza kuwa serikali imeona umuhimu wa kuanza kuzihudumia familia zinazongoja kwa kuwapatia malazi na chakula, huku kila familia ikitakiwa kuteua wawakilishi wachache tu kubaki eneo la mgodi ili kuepusha msongamano.

“Hapa kuna familia za watu 18 wanaosubiri ndugu zao kuokolewa, lakini wengine wamekuja kwa wingi. Ni hatari kukaa mgodini bila huduma za kibinadamu, hivyo tumeelekeza kila familia ibaki na watu wachache, angalau wawili, ili tuweze kuwahudumia kwa chakula na hifadhi,” alisema Mhita.

Aliongeza kuwa zoezi la uokoaji linaendelea vizuri na tayari njia za kufikia walionusurika zimeandaliwa, ikiwemo kuweka mifumo ya hewa ili kuhakikisha wanapewa msaada hadi kuokolewa.

Baadhi ya familia zilizoathirika zimeshukuru serikali kwa hatua ya kuwapatia msaada wa kibinadamu, huku zikiiomba kuharakisha uokoaji ili wapate kuungana na ndugu zao.

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code