Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 38 kutoka Nchini Uingereza, amefariki dunia baada ya kupata matatizo ya kiafya yaliyotokea ghafla wakati akijiandaa kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza nywele katika kliniki moja iliyopo Istanbul, Uturuki.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Magazeti ya Uingereza ya The Independent na The Guardian, Marehemu Martyn Latchman alikuwa akijiandaa kufanyiwa upasuaji wake wa pili katika kliniki hiyo baada ya upasuaji wake wa kwanza kufanikiwa ambapo hata hivyo kabla ya kuanza kwa mchakato wa pili, alizidiwa ghafla kwa sababu ambazo bado hazijafahamika.
Taarifa ya kliniki hiyo imesema kuwa Latchman aligundulika kuwa Mgonjwa kwa ghafla wakati wa maandalizi kabla ya upasuaji wa pili kuanza ambapo aliwaishwa katika chumba cha Wagonjwa mahututi katika hospitali ya karibu lakini alifariki dunia baadaye.
Mwili wa marehemu Latchman ambaye alihudumu kama Mwalimu Mkuu kwa zaidi ya miaka 16 huko Bedford kabla ya kubadili taaluma na kuwa Mkandarasi wa masuala ya Ulinzi, umerejeshwa Uingereza kwa uchunguzi zaidi huku Mamlaka za afya Nchini Uturuki zikianzisha uchunguzi wa kina ambapo nyaraka zote za matibabu zinazohusiana na tukio hilo zimewasilishwa kwa Mamlaka husika.
Kwa mujibu wa Baraza la Usafiri wa Matibabu Uturuki (Turkish Healthcare Travel Council), zaidi ya Watu milioni moja husafiri kila mwaka kwenda Uturuki kwa ajili ya huduma za kupandikiza nywele na vipodozi ambapo kwenye Kliniki aliyofia Latchman, imesema hadi sasa imeshafanya upasuaji mara elfu hamisini (50,000) kwa mafanikio.
image quote pre code