Ugonjwa wa malale si tatizo tena kwa nchi ya Kenya:WHO

Ugonjwa wa malale si tatizo tena kwa nchi ya Kenya:WHO

#1

Uchunguzi na ufuatiliaji wa jamii kuhusu ugonjwa wa malale unaoenezwa na mbung'o kwa wakazi wa eneo la bonde la Lambwe, Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya.



Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limetangaza rasmi Ijumaa kuwa Kenya imefanikiwa kuondoa ugonjwa wa malale au  (Human African Trypanosomiasis - HAT) kama tatizo la afya ya umma, na hivyo kuwa nchi ya 10 duniani kufikia mafanikio haya muhimu ya kiafya.

Taarifa ya WHO Kanda ya Afrika iliyotolewa Agosti 8 katika miji ya Brazaville, Congo na Nairobi, Kenya inasema malale ni ugonjwa wa tropiki unaosababishwa na vimelea vya damu vya Trypanosoma brucei, na huenezwa kwa binadamu kwa kung’atwa na mbung’o waliombukizwa vijidudu hivyo.

Aina ya ugonjwa wa malale uliokuwepo Kenya ni Rhodesiense, ambao huenea haraka na huathiri vibaya viungo mbalimbali, ikiwemo ubongo, na bila matibabu, huweza kusababisha kifo ndani ya wiki chache.

Usuli wa uamuzi wa WHO

Uamuzi huu wa WHO unakuja baada ya zaidi ya muongo mmoja bila kuripotiwa kwa mgonjwa mpya wa malale nchini Kenya. Mgonjwa wa  mwisho wa ndani ya Kenya alithibitishwa mwaka 2009, na wagonjwa wawili wa mwisho kutoka nje ni watalii wawili waliopatwa na maambukizi kwenye mbuga ya Masai Mara mwaka 2012.

Kauli ya serikali ya Kenya

“Tunasherehekea mafanikio haya kama hatua kubwa ya afya ya umma nchini mwetu,” amesema Waziri wa Afya, Dkt. Aden Duale. “Tumefanikisha hili kwa ushirikiano wa miaka mingi kati ya serikali, washirika wa maendeleo, watafiti na jamii zilizoathirika.”

Kenya iliimarisha ufuatiliaji wa malale katika vituo 12 vya afya katika kaunti 6 zilizowahi kuathirika, ikiwapa wahudumu vifaa na mafunzo ya vipimo sahihi vya ugonjwa huo. Pia, kupitia usaidizi wa mashirika ya kitaifa, nchi inaendelea kufuatilia na kudhibiti inzi wa tsetse na maambukizi kwa wanyama.

WHO imesema Kenya sasa itaanza mpango wa ufuatiliaji baada ya kutangazwa kuwa huru, kuhakikisha ugonjwa haujirudii. Dawa kwa ajili ya wagonjwa wowote wa siku zijazo zimehifadhiwa, kwa msaada wa kampuni za Bayer AG na Sanofi.

Nchi nyingine ambako malale si tishio

Kenya inaungana na nchi nyingine tisa ambazo tayari zimeondoa HAT kama tatizo la afya ya umma: Benin, Chad, Côte d’Ivoire, Equatorial Guinea, Ghana, Guinea, Rwanda, Togo, na Uganda.

Kwa sasa, jumla ya nchi 57 duniani zimefanikiwa kuondoa angalau ugonjwa mmoja wa kitropiki usiopewa kipaumbele (NTD), ikiwa ni ishara ya maendeleo ya kiafya katika maeneo yaliyoathirika kwa muda mrefu.

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code