Zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na magonjwa ya akili: WHO

Zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na magonjwa ya akili: WHO

#1

Zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na changamoto za afya ya akili kama vile msongo wa mawazo na mfadhaiko, kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa leo na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO.



Takwimu hizo zinasema mzigo huu ni wa kibinadamu na kiuchumi, huku magonjwa ya akili sasa yakiwa sababu ya pili inayoongoza kwa ulemavu wa muda mrefu.

“Kubadilisha huduma za afya ya akili ni moja ya changamoto kubwa zaidi za afya ya umma,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. “Kuwekeza katika afya ya akili ni kuwekeza kwa watu, jamii na uchumi ni uwekezaji ambao hakuna nchi inayoweza kuupuuzia.”

Kujiua ni janga la dunia miongoni mwa vijana

Ripoti hiyo inaonesha taswira ya kutisha ya matukio ya kujiua, ambapo inakadiriwa kuwa watu 727,000 walipoteza maisha mwaka 2021 pekee kwa kujiua. WHO inasema ni moja ya vyanzo vikuu vya vifo miongoni mwa vijana kote duniani, bila kujali kipato au eneo waliko.

Licha ya juhudi za kimataifa, WHO inaonya kwamba maendeleo ni ya taratibu mno ili kufikia lengo la Umoja wa Mataifa la kupunguza vifo vya kujiua kwa theluthi moja ifikapo 2030.

“Kwa mwenendo wa sasa, dunia itafanikisha upungufu wa asilimia 12 pekee,” ripoti inabainisha, ikisisitiza haja ya kuongeza kasi ya hatua.

Gharama ya trilioni ya magonjwa ya akili

Zaidi ya mateso ya kibinadamu, kwa mujibu wa ripoti athari za kifedha ni kubwa mno. Msongo wa mawazo na wasiwasi peke yake hugharimu uchumi wa dunia takriban dola za Marekani trilioni 1 kila mwaka kutokana na kupoteza uzalishaji.

Gharama za matibabu huongeza mzigo kwa familia na serikali. “Afya ya akili si suala la kiafya pekee ni suala la kiuchumi linalotishia ukuaji na uthabiti endapo litaachwa bila kushughulikiwa,” limesisitiza shirika la WHO.

Uwekezaji usio sawa na pengo linalopanuka

Ripoti hiyo “Ramani ya Afya ya Akili 2024” imeonesha hali ya kusuasua katika ufadhili. Kiwango cha kati cha serikali duniani ni asilimia 2 pekee ya bajeti za afya kinachotolewa kwa afya ya akili, kiwango ambacho hakijabadilika tangu mwaka 2017.

Tofauti ni kubwa imesema ripoti wakati nchi za kipato cha juu zinatumia hadi dola 65 kwa kila mtu, wakati nchi za kipato cha chini zinatumia senti 4 pekee. “Takwimu hizi zinaonesha ukosefu mkubwa wa usawa ambapo mamilioni wanakosa huduma kwa sababu tu ya mahali walipozaliwa,” limesema shirika la WHO.

Hatua za kisera zipo, lakini sheria bado zinasuasua

Kwa upande wa mafanikio, nchi nyingi zaidi sasa zinafanyia marekebisho sera na kuanzisha huduma za kijamii na programu za afya ya akili shuleni. Zaidi ya asilimia 80 sasa zinatoa msaada wa kisaikolojia wakati wa dharura, ikilinganishwa na asilimia 39 pekee mwaka 2020.

Hata hivyo, mageuzi ya kisheria yanayokwenda sambamba yamechelewa, WHO inasema chini ya nusu ya nchi zina sheria za afya ya akili zinazolingana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

“Bila ulinzi wa kisheria, walio hatarini zaidi huendelea kukabiliwa na unyanyapaa, kupuuzwa na hata kudhalilishwa,” ripoti imeonya.

Wito wa hatua za haraka za dunia

Wakati Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afya ya Akili na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza ukipangwa kufanyika Septemba 2025, WHO inazitaka nchi kuchukua hatua thabiti sasa. Vipaumbele ni pamoja na ufadhili wa haki, marekebisho ya kisera na kisheria, kuimarisha wataalamu wa afya ya akili, na kupanua huduma shirikishi zinazomlenga mtu.

Dk. Tedros ametoa ujumbe ulio wazi “Kila serikali na kila kiongozi ana jukumu la kuchukua hatua kwa dharura na kuhakikisha kwamba huduma za afya ya akili zinachukuliwa si kama heshima ya wachache, bali kama haki ya msingi kwa wote.”

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code