WHO Tanzania kupitia huduma za dharura za afya yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.
Katika kuhakikisha mama hapotezi maisha wakati wa kujifungua hii leo imezinduliwa miongozo mipya yenye lengo la kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake wanaofariki kila mwaka kutokana na kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua hali inayojulikana kitaalamu kama postpartum haemorrhage (PPH).
Mwongozo huo, uliozinduliwa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Shirikisho la Wakunga Duniani (ICM) na Shirikisho la Kimataifa la Madaktari wa wanawake na uzazi (FIGO) unasisitiza umuhimu wa kugundua hali hiyo mapema na kutoa matibabu ya haraka.
Takwimu zinaonesha kuwa PPH husababisha takribani vifo 45,000 kila mwaka, na kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo vya wajawazito duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema wakati wa uzinduzi huo mjini Cape Town kwamba “Leo tunasherehekea hatua muhimu katika historia ya afya ya uzazi. Katika kongamano hili, kwa kushirikiana na FIGO na ICM, WHO inajivunia kuzindua kwa pamoja mwongozo mpya wa WHO wa kukabili kutokwa damu baada ya kujifungua. Mwongozo huu unajumuisha mapendekezo 51 kuhusu chanzo hiki kikuu cha vifo vya akina mama, ukigusa maeneo ya kinga, utambuzi, matibabu na huduma saidizi. Pia umeleta ufafanuzi mpya wa kitaalamu wa PPH, ukitokana na uchambuzi mkubwa zaidi wa kimataifa wa takwimu zilizowahi kufanyika. Hii ni hatua kubwa mbele – utambuzi wa mapema, hatua za haraka, na maisha mengi zaidi kuokolewa.”
Miongozo mipya inapendekeza mabadiliko makubwa katika utambuzi wa PPH.
Watoa huduma sasa wanashauriwa kuchukua hatua haraka pindi damu inapofikia mililita 300, au dalili zisizo za kawaida za mwili zinapoonekana badala ya kungoja hadi damu ifikie mililita 500 kama ilivyokuwa awali.
Vifaa rahisi vya kupima kiwango cha damu vinapendekezwa kutumika mara moja baada ya kujifungua.
Dkt. Jeremy Farrar kutoka WHO, amesema kuwa tatizo hili “ni hatari zaidi wakati wa kujifungua kwa sababu linaweza kuongezeka kwa kasi, lakini vifo vinaweza kuzuilika kwa huduma sahihi.”
Mara tu PPH inapothibitishwa, mwongozo unapendekeza utekelezaji wa hatua zinazojulikana kama MOTIVE bundle, ikiwemo:
Kukandamiza mfuko wa uzazi,
Kutoa dawa za kuongeza mikazo ya mfuko wa uzazi,
Kutumia dawa ya kupunguza damu (tranexamic acid),
Kutoa maji kupitia mishipa ya damu,
Kuchunguza njia ya uke na sehemu ya uzazi, na
Kusogeza mgonjwa kwenye huduma ya dharura endapo kutokwa damu kunaendelea.
Profesa Anne Beatrice Kihara, Rais wa FIGO, amesema mwongozo huo “unalenga kuhakikisha wahudumu wa afya wanatoa huduma sahihi, kwa wakati sahihi, katika mazingira yote.”
Vilevile, miongozo hiyo inahimiza kuimarishwa kwa huduma za ujauzito na baada ya kujifungua, ikiwemo matibabu ya upungufu wa damu kwa kutumia madini chuma na folate, au sindano za kuongeza madini ya chuma kwa haraka inapohitajika.
Kwa upande wake, Profesa Jacqueline Dunkley-Bent wa ICM amesema, “Wakunga wanajua vyema jinsi hali hii inavyoweza kuwa hatari. Tunatoa wito kwa serikali na washirika kuwekeza zaidi katika huduma za uzazi ili PPH iwe historia.”
Mwongozo huu, uliotolewa sambamba na nyenzo za mafunzo na utekelezaji kwa ushirikiano na UNFPA, umezinduliwa rasmi katika Mkutano wa FIGO wa Dunia 2025 huko Cape Town, Afrika Kusini. Ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa malengo ya dunia ya kukomesha vifo vinavyotokana na PPH ifikapo mwaka 2030.
image quote pre code