Mataifa 65 yamesaini mkataba muhimu wa Umoja wa Mataifa mjini Hanoi, Vietnam, wenye lengo la kukabiliana na uhalifu mtandaoni hatua ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema ni “hatua ya kihistoria kuelekea dunia salama kidijitali.”
Mkataba huo, ulioidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba 2024 baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa miaka mitano, unaunda mfumo wa kwanza wa kimataifa wa kuchunguza na kufuatilia uhalifu unaotendeka mtandaoni, ikiwemo wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, programu hasidi za uchukuaji taarifa, na usambazaji wa picha za faragha bila ridhaa.
“Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu Mtandaoni ni nyenzo madhubuti na ya kisheria inayolenga kuimarisha ulinzi wetu wa pamoja dhidi ya uhalifu huu,” amesema Guterres wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo. “Ni ushahidi wa nguvu ya ushirikiano wa kimataifa, na ahadi kwamba hakuna nchi iwe tajiri au masikini itakayobaki bila kinga dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.”
Hafla hiyo iliandaliwa na Serikali ya Vietnam kwa ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Uhalifu UNODC, ikihusisha maafisa waandamizi, wanadiplomasia na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Mkataba huu mpya unaharamisha makosa mbalimbali yanayohusiana na teknolojia, unarahisisha kubadilishana ushahidi wa kielektroniki baina ya nchi, na kuanzisha mtandao wa ushirikiano wa saa 24 kwa siku kati ya Nchi wanachama.
Ni mkataba wa kwanza wa kimataifa kutambua usambazaji wa picha za faragha bila ridhaa kama kosa la jinai hatua kubwa kwa waathirika wa unyanyasaji mtandaoni.
Mkataba utaanza kutumika siku 90 baada ya nchi ya 40 kuridhia rasmi.
Ulinzi wa pamoja katika zama za kidijitali
Katika hotuba yake Guterres ameonya kuwa teknolojia, licha ya mafanikio yake, imeleta pia mianya mipya ya udhaifu.
“Kila siku, matapeli wenye ujuzi hutapeli familia, huiba riziki na kusababisha hasara ya mabilioni ya dola duniani,” alisema. “Katika dunia ya kidijitali, hakuna aliye salama hadi wote tuwe salama. Udhaifu katika eneo moja unaweza kuathiri watu na taasisi kila mahali.”
Aliongeza kuwa mkataba huo ni ushindi kwa waathirika wa unyanyasaji wa mtandaoni na unatoa mwongozo wazi kwa wachunguzi na waendesha mashtaka kuvuka vikwazo vya kisheria pale ushahidi na makosa vinapohusisha mipaka ya nchi nyingi.
Kupitia viwango vya pamoja vya ukusanyaji wa ushahidi wa kielektroniki, mkataba unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya sheria huku ukiheshimu faragha, utu na haki za binadamu.
Hafla ya kusaini ilikuwa sehemu ya ziara rasmi ya Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Vietnam, ambako alikutana na Rais Lương Cường, Waziri Mkuu Pham Minh Chinh na viongozi wengine.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Katibu Mkuu alisifu nafasi muhimu ya Vietnam katika mnyororo wa kimataifa wa teknolojia, akisisitiza umuhimu wa mataifa yote kuridhia haraka na kutekeleza mkataba huo.
“Sasa ni wakati wa kugeuza sahihi hizi kuwa vitendo,” alisema. “Mkataba huu unapaswa kuridhiwa mapema, kutekelezwa kikamilifu na kuungwa mkono kwa rasilimali, mafunzo na teknolojia, hasa kwa nchi zinazoendelea.”
Dunia salama zaidi mtandaoni
Wakati gharama za uhalifu mtandaoni zinatarajiwa kufikia zaidi ya dola trilioni 10.5 kwa mwaka 2025, mkataba huu unatoa matumaini mapya kwa mataifa, hususan yale ya Kusini kupata mafunzo, msaada wa kiufundi na ushirikiano wa haraka katika mapambano haya.
“Tuutumie wakati huu vizuri,” alihitimisha Guterres. “Tujenge mazingira ya kidijitali yanayolinda utu na haki za kila mtu, na kuhakikisha zama hizi za teknolojia zinatoa amani, usalama na ustawi kwa wote.”








image quote pre code