Unafahamu kuwa 'Love Bite' inaweza kusababisha kiharusi?

Unafahamu kuwa 'Love Bite' inaweza kusababisha kiharusi?

#1

Unafahamu kuwa 'Love Bite' inaweza kusababisha kiharusi?



Love Bite, au alama nyekundu inayotokana na busu kali kwenye ngozi huzingatiwa kama ishara ya mapenzi, mara nyingi huwekwa shingoni na alama hii inabaki mwilini kwa muda.

Lakini je, unafahamu kwamba Love Bite ambayo ni alama ya busu inayobaki shingoni inaweza kusababisha tatizo kubwa la kiafya la kiharusi?

Mnamo mwaka 2010, madaktari nchini New Zealand waliripoti kisa cha mwanamke mwenye umri wa miaka 44 aliyepata kiharusi baada ya kupata Ripoti hiyo ilieleza kuwa alama ile iligandisha damu kwenye mshipa wa carotid na kusababisha kuziba kwa mtiririko wa damu kwenda kwenye ubongo. Mwanamke huyo alipata ganzi upande mmoja wa mwili, dalili kuu ya kiharusi.

Vilevile, mwaka 2014, Jarida la Matibabu la Denmark lilichapisha ripoti ya kisa kingine cha mgonjwa aliyepata kiharusi kutokana na Love Bite. Wataalamu walieleza kuwa ingawa visa hivi ni nadra, vinaonyesha ukweli kwamba msukumo wa nguvu kwenye mishipa mikubwa ya damu unaweza kuchochea kuganda kwa damu na kuathiri ubongo.

Busu linaweza kuisisimua mishipa ya kwenye eneo la shingo 

Dokta Lameck Moses, daktari bingwa wa mifupa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini mkoani Mtwara, Tanzania, anasema kuna mishipa mikubwa ya damu ambayo inakuwa eneo la shingo na kama vitezi vidogo vikiguswa kwa kutumia nguvu au hata kwa juu juu au kwa sana, mwisho wa siku inaweza ikasababisha aidha shinikizo la damu lipande au lishuke.

Anasema kwa sababu mtu anapolibusu eneo hilo mwingine anaweza akaisisimua hiyo sehemu na kama kuna vibonge vyovyote vya damu ambavyo vipo katika eneo hilo, vinaweza vikajiachia na kwenda sehemu ya ubongo na kusababisha kiharusi.

Aidha, kitendo hicho kinaweza pia kusisimua mishipa ya fahamu iliyo kwenye shingo na kusababisha nguvu ya msukumo wa damu kupanda, hali ambayo huongeza hatari ya kuathiri mishipa ya damu ya ubongo na hata kusababisha kupasuka kwake.

''Kazi ya mishipa ya Carotids katika eneo la shingo ni kusukuma damu kupeleka kichwani na kuirudisha kwenye moyo na pia hivyo vitezi vidogo vinasaidia kufanya presha ile ya kupeleka damu kwenye ubongo na kurudisha kwenye moyo ikae kwenye vipimo vyake vya wastani,'' alifafanua Dokta Moses.

Madhara ya kupigwa busu kwa nguvu kwenye eneo la shingoni yanaweza kujitokeza mara moja baada ya tukio, au hata siku chache baadaye, hasa pale busu likiwa limewekwa chini ya kidevu au karibu na sikio. Hata hivyo, takwimu za kitabibu zinaonyesha visa hivi si vya kawaida, lakini vinapotokea vinaweza kuwa na athari kubwa kiafya.

Uelewa huo ni muhimu zaidi kwa vijana, ambao mara nyingi hushiriki kwenye vitendo hivi bila kufahamu hatari zinazoweza kujitokeza. Akizungumza na DW Kiswahili, mmoja wa wakaazi wa Mtwara Hafsa Hokororo anasema hajui kama Love Bite inaweza kusababisha ugonjwa wa kiharisu. ''Ninachofahamu mimi Love Bite ni ile sehemu ambayo imevilia damu, mtu mwingine anaweza akapata muwasho au vipele vidogo vidogo vikamtokea au hata vijipu, lakini sio kiharusi,'' alibainisha Hafsa.

Love Bite kwa vijana ni kuonyesha upendo

Kijana Lucas Edwin, kwa upande wake anasema vijana wengi sasa hivi wanajuwa kuwa Love Bite ni kama mtindo tu wa maisha au ndio kwamba ukiachiwa hiyo alama mtu unapendwa sana. ''Lakini kama inaweza kusababisha kiharusi, basi tunapaswa kuacha tu kupeana Love Bite, kwa sababu inaleta madhara makubwa katika jamii,'' alisema Edwin mkaazi pia wa Mtwara.

Madaktari wanashauri kwamba, kuonyesha mapenzi hakuhitaji kuacha alama za majeraha. Badala yake, watu watumie njia salama ambazo hazihatarishi afya zao kama kumbusu nyuma ya shingo na maeneo mengine ya mwili.

''Tunawashauri watu waache hizo tabia, kwa sababu zinaweza kuwasababishia madhara kama hayo ya kupata kiharusi ambapo kwa namna moja au nyingine wanaweza wasijuwe moja kwa moja wamepata kiharusi kwa sababu ipi,'' alisisitiza Dokta Lameck Moses.

Hata kama visa hivi ni nadra kutokea, ni vyema kujilinda na kuelimishana. Tukumbuke methali ya kiafya inayosema 'Kinga ni Bora Kuliko Tiba.' Source Dw

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code