WHO: Usugu wa bakteria dhidi ya viuavijasumu vya kawaida waenea duniani
Daktari akichambua sampuli katika maabara ya hospitali ya mafunzo nchini Nigeria
Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kuwa usugu wa bakteria dhidi ya viuavijasumu vya kawaida unaongezeka kwa kasi duniani, hali inayotishia afya ya watu na mafanikio ya tiba za kisasa.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya WHO kuhusu Usugu wa Bakteria Duniani 2025 , ambukizi moja kati ya sita lililothibitishwa maabara mwaka 2023 lilionesha usugu kwa dawa za viuavijasumu. Kati ya mwaka 2018 na 2023, zaidi ya asilimia 40 ya mchanganyiko wa bakteria na dawa ulionesha ongezeko la usugu wa wastani wa asilimia 5 hadi 15 kila mwaka.
Ripoti hiyo, iliyokusanya takwimu kutoka zaidi ya nchi 100 kupitia mfumo wa ufuatiliaji ujulikanao kama Global Antimicrobial Resistance and Use Surveillance System au GLASS, inaonesha kuwa usugu wa dawa ni mkubwa zaidi katika kanda za Kusini-Mashariki mwa Asia na Mediterania ya Mashariki, ambako maambukizi moja kati ya matatu hayaitikii tiba. Katika Bara la Afrika, maambukizi moja kati ya matano yanaonesha usugu huo.
Katika taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi kuhusu ripoti hiyo imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, akisema kuwa “Usugu wa viuavijasumu unatangulia maendeleo ya tiba za kisasa na unatishia afya ya familia kote duniani. Tunapaswa kutumia dawa kwa uangalifu, kuboresha uchunguzi, na kuwekeza katika tiba na chanjo mpya.”
Aina za Bakteria
WHO imesema bakteria aina ya “Gram-negative” kama E. coli na Klebsiella pneumoniae ndiyo tishio kubwa zaidi, hasa katika maambukizi ya damu ambayo mara nyingi husababisha viongo vya mwili kushindwa kufanya kazi na kifo.
Utafiti umegundua zaidi ya asilimia 40 ya E. coli na asilimia 55 ya K. pneumoniae duniani sasa hazikubali kutibika kwa dawa za kizazi cha tatu za cephalosporins ambayo ndio tiba ya kwanza ya maambukizi hayo. Nchini za Afrika, usugu huo unazidi asilimia 70.
Ongezeko la nchi
Pamoja na changamoto hizo, WHO imepongeza maendeleo katika ufuatiliaji wa usugu wa viajivyasumu ikisema idadi ya nchi zinazoshiriki kufanya ufuatiliaji imeongezeka kutoka 25 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2023. Hata hivyo, nchi nyingi bado hazina uwezo wa kukusanya na kuripoti takwimu sahihi.
WHO inazitaka nchi zote kuimarisha maabara, kufuatilia matumizi ya dawa, na kutoa taarifa kamili kuhusu usugu wa viuavijasumu ifikapo mwaka 2030, ili kuwezesha sera bora na tiba zenye ufanisi zaidi.
image quote pre code