Aimé Manga ni Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, anayewahudumia wanawake waliobakwa katika vita huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wakati mji wa Goma ukijaribu kurejea katika hali ya utulivu, vita nyingine inaendelea kimyakimya, vita ya ukatili wa kingono. Katika vitongoji vya pembezoni mwa jiji, ambako usalama bado sio wa uhakika, wanawake wengi wanaendelea kupitia mateso ya ukatili wa hali ya juu, ikiwemo kubakwa na hata kukeketwa sehemu za siri. Ukatili huu, unaofanywa mara nyingi usiku na watu wenye silaha, umeacha nyuma yake majeraha ya miili na nafsi zilizovunjika.
Daktari Aimé Manga amejipa jukumu la kurekebisha yale ambayo vita imeharibu. Ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Rehema mjini Goma, anayewatibu bure waathirika wa ukatili wa kingono na wanawake waliokeketwa.
Katika Hospitali ya Rehema, Dokta Aimé Manga huwapokea wanawake waliobakwa na walioumizwa. Yeye ameamua kujitolea kikamilifu kurejesha afya ya miili na nafsi zao, bila malipo, bila ufadhili, na yote hayo kwa moyo wa kibinadamu tu.
"Hata sisi madaktari, kwa namna fulani, tumepata mshtuko wa kisaikolojia. Lakini tufanye nini? Tunapokuwa tukiwatibu hawa wanawake, tunafanya kwa umakini mkubwa kwa sababu tunajiambia, ni sasa au kamwe, '' alisema Daktari Manga.









image quote pre code