HESLB yatoa bil 215.3/- kwa wanafunzi 66,987

HESLB yatoa bil 215.3/- kwa wanafunzi 66,987

#1

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza rasmi awamu ya pili ya upangaji wa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa vyuo ambapo wanafunzi 66,987 wamepangiwa kiasi cha Sh bilioni 215.3.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa juzi.

Alisema wanafunzi waliopangiwa mikopo na ruzuku katika awamu hiyo ni 43,562 wa shahada ya awali na wanafunzi 1,179 wa stashahada wamepangiwa mikopo ya Sh bilioni 143.7.

Dk Kiwia alisema wanafunzi 288 wa Samia Skolashipu wamepangiwa ruzuku ya Sh milioni 575 na wanafunzi 230 wa Shule ya Sheria Tanzania wamepangiwa Sh bilioni 1.5.

Alisema wanafunzi 21,729 wanaoendelea na masomo wameruhusiwa kupata mikopo na ruzuku ya Sh bilioni 69.4 baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka uliotangulia.

“Hadi sasa, HESLB imemaliza upangaji wa mikopo kwa wanafunzi 202,227 ya thamani ya Sh bilioni 641.8 kati ya Sh bilioni 916.7 zilizotengwa na serikali kwa mwaka wa masomo 2025/2026,” alisema Dk Kiwia kwenye taarifa hiyo.

Alisema bodi hiyo inawataka wanafunzi ambao hawajafanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu zote mbili na wale walio na taarifa za ziada ambazo hawakuweza kuwasilisha wakati wa maombi, kuanza kukata rufaa.

“Dirisha la rufaa litafunguliwa kuanzia kesho Novemba 10 hadi 17, 2025 na maelekezo ya kukata rufaa yanapatikana katika akaunti binafsi ya mwombaji,” alisema.

Alisema bodi hiyo inasisitiza kuwa itendelea kupanga mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo kadiri itakavyopokea matokeo kutoka vyuoni.

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code