Ni mtu mmoja tu kati ya watu milioni sita mwenye aina nadra sana ya damu iitwayo Rh null. Sasa watafiti wanajaribu kuizalisha katika maabara, wakitumaini kuwa siku moja itaweza kuokoa maisha.
Utoaji wa damu umeleta mageuzi makubwa katika tiba za kisasa. Iwapo mtu atapata jeraha au kuhitaji upasuaji mkubwa, damu iliyotolewa na wengine huweza kuwa tiba ya kuokoa uhai.
Hata hivyo, si kila mtu anayefaidi na huduma hii muhimu. Watu wenye aina adimu za damu mara nyingi hupata shida kubwa kutafuta damu inayooana na yao.
Miongoni mwa aina adimu zaidi duniani ni Rh null, inayopatikana kwa watu 50 tu wanaojulikana.
Iwapo mtu mwenye aina hii atapata ajali inayohitaji damu, nafasi ya kuipata inayooana na hiyo ni ndogo sana.
Kwa sababu hii, hushauriwa kugandisha damu yao wenyewe kwa matumizi ya baadaye.
Lakini licha ya nadra yake, aina hii pia inathaminiwa sana na wanasayansi.
Katika ulimwengu wa tiba na utafiti, mara nyingi huitwa "damu ya dhahabu" kwa sababu ya matumizi yake ya kipekee.
Inaweza pia kusaidia kufanikisha ndoto ya kuunda damu ya ulimwengu mzima (universal blood) damu inayoweza kutolewa kwa karibu kila mtu bila hatari ya mwitikio wa kinga.
Watu watatu wamesimama wakiwa watoto wachanga waliochorwa ukutani. Mchoro inaonyesha mikono miwili mikubwa, moja nyekundu na moja ya chungwa iliyoshikilia maumbo na aina za damu zimeandikwa "A, B, AB, na O" ndani yake.
Kwa nini aina ya damu hutofautiana
Aina ya damu huamuliwa na uwepo au kutokuwepo kwa alama maalum (antijeni) kwenye uso wa seli nyekundu. Hizi ni protini au sukari zinazotambulika na mfumo wa kinga.
"Ukipokea damu yenye antijeni tofauti na zako, mwili hutengeneza kingamwili kuzishambulia," anaeleza Profesa Ash Toye wa Chuo Kikuu cha Bristol. "Ukipokea tena damu ya aina hiyo, madhara yake yanaweza kuwa hatari."
Mifumo mikuu inayosababisha mwitikio mkubwa wa kinga ni ABO na Rhesus (Rh).
A ina antijeni A
B ina antijeni B
AB ina yote
O haina yoyote
Kila moja inaweza kuwa Rh chanya au hasi.
Watu wa O hasi mara nyingi huonekana kama wachangiaji wa "kila mtu", lakini hili si sahihi kikamilifu.
Kufikia 2024 kulikuwa na zaidi ya makundi 47 ya damu na antijeni 366, hivyo mtu wa O hasi bado anaweza kupata mwitikio wa kinga kutokana na antijeni nyingine.
Zaidi ya hapo, pia kuna zaidi ya antijeni 50 za Rh.
Hivyo, mtu anaposema ni Rh hasi, kwa kawaida huashiria tu antijeni Rh(D), huku nyingine zikiendelea kuwepo.
Pia kuna aina mbalimbali za antijeni za Rh duniani kote, hivyo kufanya iwe vigumu kupata zinazolingana na wafadhili wa kweli, hasa kwa watu kutoka asili za makabila madogo katika nchi fulani.
Mkono wenye glavu umeshikilia slaidi ya glasi yenye matone ya damu yakipimwa, ikionyesha sampuli zenye rangi tofauti na miitikioChanzo cha picha,Getty Images
Maelezo ya picha,Aina ya damu ya Rh null hupatikana katika watu 50 tu wanaojulikana ulimwenguni
Watu wenye Rh null hawana antijeni zote 50 za Rh.
Kwa hiyo hawawezi kupokea aina nyingine ya damu, lakini damu yao inaweza kupewa karibu watu wote wenye aina tofauti za Rh.
Ikiwa mtu ana O Rh null, damu yake huwa ya thamani sana kwa kuwa inaweza kutolewa kwa watu wengi sana, ikiwemo wale wenye aina zote za ABO.
Katika dharura ambapo aina ya damu ya mgonjwa haijulikani, O Rh null inaweza kutolewa kwa hatari ndogo ya mzio.
Hii ndiyo sababu wanasayansi duniani kote wanajaribu kuizalisha maabara.
"Rh [antijeni huchochea] mwitikio mkubwa wa kinga na kwa hivyo ikiwa huna [yao] kabisa basi kimsingi hakuna kitu cha kuguswa nayo katika suala la Rh," asema Prof Toye.
"Kama ungekuwa aina ya O na Rh null basi hilo ni jambo la kawaida kabisa. Lakini bado kuna makundi mengine ya damu ambayo bado unapaswa kuzingatia."
Asili ya aina ya damu ya Rh null
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa Rh null husababishwa na mabadiliko ya jeni yanayoathiri protini muhimu iitwayo RHAG, ambayo husaidia uundaji wa antijeni za Rh.
Mabadiliko hadi kwenye protini hii huvuruga kutengenezwa kwa antijeni nyingine za Rh.
Mwaka 2018, Prof. Toye na timu yake walifanikiwa kuunda damu ya Rh null maabara kwa kutumia teknolojia ya Crispr-Cas9 kufuta jeni za antijeni za makundi matano makuu yanayosababisha kutopatana kwa damu: ABO, Rh, Kell, Duffy na GPB.
"Tulisuluhisha ikiwa tutaondoa tano, basi hiyo ingeunda seli inayolingana kabisa, kwa sababu ilikuwa na vikundi vitano vya damu vilivyo na shida zaidi vilivyoondolewa," anasema Prof Toye.
Kwa kufanya hivyo waliunda seli zilizo sambamba na makundi yote makubwa ya damu, ikiwemo aina adimu kama Rh null na Bombay phenotype, aina nyingine nadra sana inayopatikana kwa mtu mmoja kati ya watu milioni nne.
Watu walio na kundi hili la damu hawawezi kupewa O, A, B au AB damu.
Hata hivyo, matumizi ya uhariri wa jeni bado yamezuiliwa na sheria kali katika nchi nyingi, hivyo huenda ikachukua muda mrefu kabla ya damu hii kupitishwa kwa matumizi ya hospitali.
Juhudi za kutengeneza damu ya maabara
Professa Toye ameshaunda kampuni ijulikanayo kama Scarlet Therapeutics, inayokusanya damu kutoka kwa watu wenye aina adimu za damu kwa ajili ya kuunda mistari ya seli itakayoweza kuzalisha seli nyekundu bila kikomo.
Damu hii inaweza kugandishwa kwa matumizi ya dharura.
"Ikiwa tunaweza kuifanya bila kuhariri, basi ni nzuri, lakini kuhariri ni chaguo kwetu," anasema.
"Sehemu ya kile tunachofanya ni kuchagua wafadhili kwa uangalifu kujaribu kufanya antijeni zao zote ziendane iwezekanavyo kwa watu wengi. Kisha pengine itatubidi kuhariri jeni ili kuifanya iendane na kila mtu." Via:BBC









image quote pre code