Profesa Mohamed Janabi, ametahadharisha akisema dawa ambazo hapo awali ziliokoa maisha sasa hazifanyi kazi

Profesa Mohamed Janabi, ametahadharisha akisema dawa ambazo hapo awali ziliokoa maisha sasa hazifanyi kazi

#1

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO Kanda ya Afrika Dkt.Mohamed Yakub Janabi

Usugu dhidi ya Viua-Vijasumu (AMR)unaelezwa kama janga la kimyakimya linalotishia kurudisha nyuma mafanikio ya miongo kadhaa katika tiba na afya. Tunapoadhimisha Wiki ya Kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu usugu dhidi ya Viua-Vijasumu au antibiotics, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, ametahadharisha akisema dawa ambazo hapo awali ziliokoa maisha sasa hazifanyi kazi kama ilivyokuwa na hivyo inabidi kuchukua hatua za pamoja na haraka.

“Kanda yetu ndiyo iliyoathirika zaidi duniani,” anasema Prof. Janabi na kufafanua zaidi kwamba, “Watu ishirini na saba nukta tatu kati ya kila watu laki moja hufariki dunia kutokana na upinzani dhidi ya viua-vijasumu. Iwapo hakuna hatua itakayochukuliwa kufikia mwaka 2050, kwa pamoja tutapoteza watu milioni sita.”

Daktari huyo anayeongoza ofisi ya WHO Kanda ya Afrika anaongeza kuwa hatari hii mara nyingi haionekani wazi, lakini madhara yake yanaweza kuwa makubwa sana.

Usugu dhidi ya Viua-Vijasumu hutokea pale bakteria, virusi, kuvu na vimelea wanapobadilika na kufanya dawa zilizotumika awali kuwadhibiti kutofanya kazi.

Kwa mujibu wa WHO, tatizo hili linazidi kuwa kubwa kutokana na matumizi mabaya au kupita kiasi ya viua-vijasumu, ukosefu wa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji, pamoja na udhaifu katika sheria na udhibiti wa dawa, changamoto ambazo bado zimesambaa katika maeneo mengi ya Afrika.

Profesa Janabi pia ameeleza wasiwasi kuhusu mapungufu makubwa ya takwimu akisema “Ni asilimia 40 tu ya nchi za Afrika zilizo na mifumo thabiti ya kukusanya na kuchakata data za Usugu dhidi ya Viua-Vijasumu, AMR.

“Kile ambacho sasa WHO inajaribu ni kuhakikisha nchi zote arobaini na saba wanachama zinatengeneza hazina kamili za taarifa,” anaeleza. “Nina hakika takwimu hizi zitakuwa mara mbili au tatu zaidi. Ndiyo maana ni muhimu sana kwetu kama taasisi inayoongoza masuala ya afya kuwa na wasiwasi mkubwa.”

Wataalamu wa afya wanasema bila hatua za haraka kama vile kuimarisha kinga dhidi ya maambukizi, kuboresha mifumo ya afya na kutumia viua-vijasumu kwa uangalifu, Afrika inakabiliwa na hatari ya siku zijazo ambako hata maambukizi ya kawaida hayatakuwa na tiba.

WHO inazitaka serikali, wahudumu wa afya na jamii kushirikiana kulinda mustakabali wa bara na kizazi kijacho.

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code