Polisi Mwanza waanza uchunguzi moto kuunguza mabweni Sekondari ya Sumve.
Polisi Mwanza waanza uchunguzi moto kuunguza mabweni Sekondari ya Sumve.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali, limeanza uchunguzi kuhusu tukio la moto lililotokea Novemba 20, 2025 majira ya saa 7:13 mchana katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Sumve, iliyopo Kitongoji cha Sumve, Kata ya Sumve, Tarafa ya Ngula, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, moto huo mkubwa ulizuka wakati wanafunzi wakiwa madarasani wakiendelea na masomo na kuteketeza mabweni mawili ya wasichana yanayojulikana kwa majina ya Nkwame na Dr. Magufuli.
Inadaiwa kuwa moto huo ulisambaa kwa kasi kutokana na uwepo wa vifaa vinavyowaka haraka ikiwemo magodoro, nguo, mablanketi na mali nyingine za wanafunzi waliokuwa wakiishi katika mabweni hayo. Aidha, hakuna mtu yeyote aliyepata madhara na chanzo cha tukio hicho kinaendelea kuchunguzwa.
Mara baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi, walifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto kabla haujasababisha madhara zaidi. Baadhi ya mali ziliokolewa zikiwemo magodoro, matranka, mablanketi, ndoo za maji na viatu.
Kwa sasa uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo unaendelea, na ulinzi umeimarishwa katika shule hiyo pamoja na shule jirani, kwa ushirikiano na wananchi na uongozi wa shule.
Kamanda Mtafungwa ametoa wito kwa wananchi wote wenye taarifa zinazoweza kusaidia kubaini chanzo cha tukio hilo kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha uchunguzi.












image quote pre code