Katika dunia ambayo tayari takribani mwanamke mmoja kati ya watatu hupitia ukatili wa kimwili au kingono, kuenea kwa teknolojia za Akili Mnemba AI, kumeongeza kwa kiasi kikubwa wigo, kasi na ukali wa ukatili unaofanyika mtandaoni.
Zana nyingi za AI zimejengwa juu ya mifumo inayobeba au kuendeleza upendeleo wa kijinsia. Matokeo yake, teknolojia hizi zimezalisha aina mpya za unyanyasaji wa kidijitali na kuimarisha zile zilizokuwepo, hali ambayo wataalamu wanaielezea kama “dhoruba kamili ya madhara.”
Ukatili wa kidijitali unaongezeka kwa kasi
Tafiti zinaonesha kuwa kati ya asilimia 16 hadi 58 ya wanawake duniani wamewahi kukumbwa na ukatili unaochochewa na teknolojia. Ujio wa AI umeharakisha zaidi ongezeko hilo.
Matokeo ya utafiti mmoja wa kimataifa yanaonesha kuwa:
Asilimia 38 ya wanawake wamewahi kushambuliwa mtandaoni moja kwa moja.
Asilimia 85 wamewahi kushuhudia ukatili huo ukiwalenga wanawake wengine.
Madhara ya mtandaoni mara nyingi hupenya kwenye maisha halisi, na kusababisha athari mbaya za kimwili, kiakili, kiuchumi na kijamii.
Aidha, wataalamu wameonya kuwa zana nyingi zinazotengeneza picha bandia za Akili Mnemba zenye maudhui ya ngono huundwa na timu za wanaume pekee, na baadhi ya programu hizo hufeli kufanya kazi kwenye miili ya wanaume jambo linalodhihirisha mizizi ya ubaguzi wa kijinsia katika uundaji wa teknolojia za kisasa.
Katika mahojiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women), wanaharakati wa haki za wanawake Laura Bates mwandishi wa "Enzi Mpya ya Ubaguzi wa Kijinsia" pamoja na mtaalamu wa sera za teknolojia Paola Gálvez-Callirgos, wameeleza ukubwa wa hatari inayoongezeka.
Watoto wengi wanakabiliwa na unyanyasaji mtandaoni.
Ukatili unaochochewa na AI ni nini?
Ni aina ya unyanyasaji wa kidijitali unaozalishwa, kuendelezwa au kusambazwa kwa kutumia teknolojia za AI, na unaosababisha madhara ya kingono, kimwili, kisaikolojia, kijamii, kisiasa au kiuchumi kwa wanawake na wasichana.
Kwa sababu ya kasi yake, ueneaji mpana na urahisi wa kujificha mtandaoni, wahalifu hujihisi hawaguswi. Wakati huohuo, mifumo ya kisheria mara nyingi hushindwa kwenda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia.
Laura Bates anasisitiza kuwa “mgawanyiko kati ya maisha ya mtandaoni na maisha halisi haupo.”
Anataja mifano kama:
Wanyanyasaji wa majumbani kufuatilia mienendo ya waathiriwa kupitia zana za kiteknolojia;
Taswira bandia za AI zenye maudhui ya ngono kusababisha wanawake kupoteza ajira au nafasi ya kulea watoto;
Wasichana kuacha masomo kwa sababu ya fedheha inayosambazwa mtandaoni.
Je, AI inaibua aina mpya za ukatili?
Ndiyo. AI imezalisha aina mpya za ukatili wa kijinsia mtandaoni huku pia ikiongeza ukubwa wa zile zilizokuwepo.
1. Picha zenye taswira bandia zenye maudhui ya ngono zilizobadilishwa kwa AI hadi kuonekana halisi.
Takwimu muhimu:
90–95% ya picha bandia za AI mtandaoni ni maudhui ya ngono yasiyoridhiwa.
90% ya waathiriwa ni wanawake.
Mwaka 2023 kulikuwa na ongezeko la 550% la taswira bandia kulinganisha na 2019.
98% ya taswira bandia zote mtandaoni zina maudhui ya ngono.
Zana hizi hutumiwa kuwadhuru wanawake kihisia, kijamii na kiuchumi kwa sababu zinatengenezwa kwa urahisi, kusambaa haraka na mara nyingi haziwezi kufutwa kabisa.
2. Utambulisho bandia na udanganyifu wa kingono
AI sasa inaweza kutengeneza sura, sauti na tabia za mtu bandia zinazoweza kuzungumza kama binadamu halisi. Wahalifu hutumia mbinu hizi:
kuwadanganya wanawake kutoa taarifa binafsi,
kuanzisha uhusiano bandia,
au kuwalaghai wakutane nao bila kujua kuwa wanawasiliana na mashine.
3. Ufichuaji hatarishi wa taarifa binafsi
Zana za AI zinaweza kuchanganua machapisho ya wanawake mtandaoni—hasa yale ya kulaani ukatili wa kijinsia—na kuyafanya walengwe zaidi na mashambulizi.
Baadhi ya mifumo ya AI hutengeneza ujumbe wa vitisho ulio maalum kwa kutumia taarifa au maneno ya mhanga mwenyewe.
Kwa nini wanawake ndio wahanga wakuu wa taswira bandia za AI?
Taswira bandia za AI ni picha, video au sauti zilizobadilishwa kwa akili mnemba ili kuonekana kama mtu amesema au kufanya jambo ambalo hakufanya.
Ingawa zinaweza kutumika katika sanaa na burudani, leo zimetumika zaidi kama silaha ya kudhalilisha wanawake.
Laura Bates anaeleza kuwa mizizi ya tatizo iko kwenye mifumo ya kijamii inayojenga na kuendeleza chuki dhidi ya wanawake:
“Huu ni ukatili wenye sura ya kidijitali unaoakisi ubaguzi wa kijinsia wa maisha halisi.”
Msaada wa haraka: Nini cha kufanya ndani ya saa 24?
StopNCII.org – Hii ni wavuti ambayo husaidia kuzuia kusambazwa kwa picha za faragha.
Chayn Global Directory – Orodha ya mashirika yanayosaidia manusura wa ukatili wa kijinsia.
Online Harassment Field Manual – Huu ni mwongozo hutoa ushauri wa usalama mtandaoni, mbinu za kujilinda dhidi ya unyanyasaji na namba muhimu za dharura.
Cybersmile Foundation –Shirika hili hutoa msaada wa kisaikolojia na ushauri kwa watu wanaopitia unyanyasaji wa mtandaoni.
Take It Down – Ni huduma salama ya mtandaoni inayosaidia kuondoa picha au video za utupu mtandaoni.
Sheria zinazolinda wanawake dhidi ya ukatili unaotokana na AI
Baadhi ya nchi zimeweka sheria, ingawa utekelezaji bado ni changamoto.
Mifano:
Uingereza – Sheria ya Usalama Mtandaoni (2023): Inakataza kusambaza picha bandia za ngono, ingawa haijajikita sana kwenye utengenezaji wake.
Umoja wa Ulaya – Sheria ya AI (2024): Inahitaji maudhui yote yaliyotengenezwa na AI yawekwe alama za utambulisho.
Mexico – Ley Olimpia: Inatambua na kuadhibu ukatili wa kidijitali.
Australia: Inaendelea kuandaa sheria kali za kuzuia utengenezaji na usambazaji wa picha za ngono bandia.
Wataalamu wanasisitiza haja ya viwango vya kimataifa na uwajibikaji wa kampuni za teknolojia.
Wajibu wa makampuni ya teknolojia
Kampuni za teknolojia zinapaswa:
Kuzuia upatikanaji wa zana zinazozalisha taswira bandia za ngono.
Kuondoa na kutokuruhusu kuhifadhi maudhui hayo kwenye majukwaa yao.
Kurahisisha njia za kuripoti ukatili mtandaoni.
Kutumia teknolojia za kubaini maudhui bandia.
Kuweka alama za utambulisho kwa yaliyotengenezwa na AI.
Kuongeza idadi ya wanawake katika uundaji wa zana za kiteknolojia.
Akili Mnemba na uenezaji wa itikadi za chuki dhidi ya wanawake
Laura Bates anataja uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya AI na kuenea kwa mawazo ya chuki dhidi ya wanawake yanayotoka katika jumuiya za mtandaoni zinazojulikana kama Manosphere.
Jumuiya hizi hutumia AI kueneza:
- Taarifa potofu,
- takwimu feki,
- simulizi zinazochochea ubaguzi wa kijinsia.
Mambo matatu ya kuzingatia ili kuwa salama mtandaoni
1. Jielimishe na elimisha wengine kuhusu usalama wa mtandaoni na namna teknolojia hutumiwa vibaya.
2. Jilinde kwa kutumia nywila thabiti, uthibitishaji wa hatua mbili na mipangilio ya faragha.
3. Chukua hatua kwa kudai uwajibikaji wa kampuni za teknolojia na kuunga mkono juhudi za kutetea haki za wanawake. Via UN









image quote pre code