Kituo cha Kimbilio Salama (Kimbilio Women Center) kilichopo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, kimefanikiwa kuwaokoa wasichana takribani 89 waliokuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo ndoa za utotoni, kubakwa na kunyimwa haki ya kupata elimu.
Wasichana hao waliokolewa kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro na hata nje ya mkoa huo, ambapo wamekuwa wakihifadhiwa, kutunzwa na kupewa msaada wa kisheria na kijamii katika kituo hicho.
Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Mchungaji Norbert Mbwillo, alisema hayo alipokuwa akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, walipotembelewa na ujumbe kutoka Usharika wa Lempaala Nemc nchini Finland — ambao ndio wafadhili wakuu wa kituo hicho.
Mchungaji Mbwillo alieleza kuwa kituo hicho kilianza mwaka 2017 mjini Morogoro kwa lengo la kusaidia watoto wa kike wanaokumbwa na matatizo ya kijamii, likiwa chini ya ufadhili wa washirika hao wa Finland.
Alibainisha kuwa, idadi kubwa ya wasichana wanaookolewa hutoka wilaya ya Mvomero, ikifuatiwa na Kilosa, huku wachache wakitoka Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine nje ya mkoa.
“Kituo chetu kinapokea wasichana wote wanaofanyiwa ukatili bila kujali dini au kabila. Tunawasaidia waliobakwa, waliolazimishwa kuolewa wakiwa watoto, na wale waliokatishwa masomo yao,” alisema Mchungaji Mbwillo.
Alifafanua kuwa kabla ya kupokelewa, matukio ya ukatili huripotiwa kwanza Polisi, kisha wahusika hukabidhiwa kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ambayo huwaleta rasmi kituoni hapo.
Kwa mujibu wa Mchungaji Mbwillo, Kituo cha Kimbilio Salama kimekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Morogoro kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa waathiriwa na kufuatilia kesi zao hadi mahakamani.
“Baadhi ya watoto hawa wamebakwa na wazazi wao wenyewe. Tumeshughulikia kesi nyingi, ikiwemo tatu ambazo wahanga walibakwa na baba zao, na mmoja wao alijifungua mtoto aliyefariki muda mfupi baada ya kuzaliwa,” alisema kwa masikitiko.
Amesema msaada mkubwa wa uendeshaji wa kituo hicho unatolewa na marafiki kutoka Finland na waumini wa Dayosisi ya Morogoro.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Askofu Mteule wa Dayosisi ya Morogoro, Mchungaji Peter Makalla, alisisitiza umuhimu wa jamii kukemea ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike, akitoa wito kwa wananchi “kupaza sauti ili wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao na taaluma zao kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, akisisitiza kuwa wanawake na watoto wa kike wanapaswa kupata haki zao za msingi ili kujenga taifa lenye usawa na utu.









image quote pre code