Watu 7 wafariki El-Fasher Sudan kufuatia shambulizi la droni hospitali ya Watoto

Watu 7 wafariki El-Fasher Sudan kufuatia shambulizi la droni hospitali ya Watoto

#1

Watu saba wameuwawa katika shambulizi la droni lililofanywa katika hospitali ya watoto nchini Sudan.

Haya ni kwa mujibu wa madaktari katika taifa hilo lililozongwa na mapigano.

Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouwawa kwenye shambulizi hilo lililofanywa eneo la Kernoi karibu kilomita 270 kutoka mji wa El-Fasher katika eneo la Darfur.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan wanasema wanamgambo wa RSF ndio waliofanya shambulizi hilo katika eneo hilo lililo karibu na mpaka wa Chad.

Wiki iliyopita wanamgambo wa RSF waliripotiwa kuwauwa zaidi ya wagonjwa 460 pamoja na jamaa zao katika hospitali moja ya kina mama wajawazito kujifungua, baada ya kuuteka mji wa El-Fasher.

El-Fasher yakabiliwa na njaa na inaenea maeneo mengine

Wakati huo huo kundi la uangalizi wa njaa duniani IPC limesema kuwa maeneo mawili ya Sudan yanakabiliwa na njaa ambayo iko kwenye hatari ya kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

IPC inasema kuna njaa katika eneo la El-Fasher huko magharibi mwa Darfur na katika mji wa Kadugli ulioko katika mkoa wa South Kordofan.

Kulingana na shirika hilo, njaa hiyo pia inatishia maeneo mengine ambayo mapigano yamekithiri.

Hayo yakiarifiwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, imeonya kuwa ukatili unaofanywa huko El-Fasher, unaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.  

ICC imeyasema haya baada ya Umoja wa Mataifa kudai kuwa maelfu ya watu wamelikimbia eneo jirani na El-Fasher ambalo limetekwa na wanamgambo wa RSF kwa sasa.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa,zaidi ya watu 36,000 wameikimbia miji na vijiji katika eneo ka Kordofan kati ya Oktoba 26 na Ijumaa iliyopita.

Kumeripotiwa ongezeko la wanamgambo wa RSFna wanajeshi wa Sudan katika miji na vijiji vilivyoko katika jimbo la North Kordofan.

Wanamgambo wa RSF waliuzingira mji wa El-Fasher kwa miezi 18 na kukata njia zote za makumi kwa maelfu ya watu kupata chakula na bidhaa zengine muhimu.

Pande hizo mbili zinalipigania eneo la El-Obeid kwa sasa, ambao ndio mji mkuu wa jimbo la North Kordofan na mji muhimu wa kibiashara unaoiunganisha Darfur na Khartoum.

Mashambulizi baada ya kukataliwa kujiunga na jeshi

Wanamgambo hao walianza kulishambulia jeshi la Sudan na raia mwezi Aprili mwaka 2023 kwasababu walinyimwa nafasi ya kujumuishwa kwenye jeshi la nchi hiyo.

Kutokea wakati huo, wamefanikiwa kuliteka karibu eneo zima la Darfur magharibi na wanatuhumiwa kufanya mauaji makubwa, ubakaji na kuwafurusha watu kutoka kwenye maeneo yao kwa misingi ya kikabila.

Jeshi la Sudan nalo pia linatuhumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita kama kurusha mabomu katika maeneo yaliyo na raia.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa hali iliyosababishwa na vita vinavyoendelea vimeufanya mzozo huo wa Sudan kuwa mbaya zaidi duniani.

Vyanzo: DPA/AFP

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code