Tarehe 18 - 24 Novemba: Wiki ya Kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu usugu wa vijiumbemaradhi dhidi ya dawa
Usugu wa dawa za viuavijumbemaradhi (AMR) unatishia uzuiaji thabiti na matibabu ya maambukizi yanayosababishwa na vijidudu mbalimbalimbali.
Picha: WHO Usugu wa dawa za viuavijumbemaradhi (AMR) unatishia uzuiaji thabiti na matibabu ya maambukizi yanayosababishwa na vijidudu mbalimbalimbali.
Kuanzia jana tarehe 18 inaanza Wiki ya Kimataifa ya Kuelimisha Umma kuhusu Usugu wa Vijiumbemaradhi dhidi ya dawa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, linaonya kuwa usugu wa vimelea vya magonjwatayari unatishia mifumo ya afya, uchumi na uhakika wa chakula.
Kwa kaulimbiu “Chukua Hatua Sasa: Linda Leo Yetu, Linda Mustakabali Wetu,” WHO inatoa wito kwa serikali, wahudumu wa afya, wakulima, wadau wa mazingira na umma kuchukua hatua madhubuti kutekeleza ahadi za kisiasa ili kupunguza kuenea kwa maambukizi sugu ya dawa. Wiki hii itaendelea hadi tarehe 24 japokuwa uelimishaji umma kuhusu tatizo hili la usugu wa magonjwa ni jambo endelevu.
Usugu wa vijumbemaradhi, au AMR, hutokea pale bakteria, virusi, fangasi na vimelea wanapobadilika na kutoitikia tena dawa. Wataalamu wa afya wanaonya kuwa hali hii inafanya maambukizi kuwa magumu zaidi kutibu na inaongeza hatari ya kusambaa kwa magonjwa, kusababisha ugonjwa mkali na hata vifo. Kadri viua vijasumu na dawa nyingine zinavyopoteza ufanisi, maambukizi yaliyokuwa rahisi kutibu hapo awali yanaweza kuwa hatari zaidi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa AMR imekuwa ikiongezeka kwa miongo kadhaa, kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi mabaya au kupindukia ya viua vijasumu kwa binadamu, wanyama na katika kilimo. Kutokana na hilo, mpango wa kimataifa wa kukabiliana na AMR uliidhinishwa na Baraza la Afya Duniani mwaka 2015, ukilenga kuboresha ufuatiliaji, matumizi sahihi ya dawa na kuongeza uelewa wa umma.
Moja ya nguzo kuu za mpango huo ni mawasilianona hapa ndipo wiki hii inapochukua nafasi yake. Kampeni hii ya kila mwaka inalenga kuongeza uelewa kuhusu usugu kwa dawa na kuhamasisha tabia bora miongoni mwa umma, watunga sera na wadau wote wa “One Health,” wakiwemo wahudumu wa afya ya binadamu, afya ya wanyama na mazingira.
Mamlaka za afya zinasisitiza kuwa kupunguza AMR kunahitaji uwajibikaji wa pamoja. Matumizi sahihi ya viua vijasumu, usafi, chanjo na mifumo imara ya afya ni muhimu katika kuzuia maambukizi na kupunguza kasi ya ueneaji wa AMR.
Kadri maadhimisho ya mwaka huu yanavyoendelea, mashirika ya afya duniani yanatoa wito kwa serikali, wataalamu na jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya AMR, yakionya kwamba bila hatua za pamoja, dunia inaweza kuelekea katika enzi mpya ambapo maambukizi rahisi yanaweza tena kuwa hatari na kusababisha vifo.









image quote pre code