WHO:Aina mpya ya homa ya mafua inaongezeka kwa kasi, lakini chanjo bado ni kinga bora
Muguzi mwenye tabasamu na mama aliye na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minane kwenye kituo cha afya huko Kyiv, Ukrainia, akijitayarisha kwa ajili ya chanjo.
Wakati msimu wa homa ya mafua katika Ulimwengu wa Kaskazini ukianza mapema, aina mpya ya virusi inaenea kwa kasi hata hivyo, chanjo bado ndio “ulinzi wenye ufanisi zaidi”, limesema leo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO.
Homa ya mafua na virusi vingine vya mfumo wa kupumua vinaongezeka, amesema Dkt. Wenqing Zhang, Mkuu wa Kitengo cha Vitisho vya Kimataifa vya Magonjwa ya Njia ya mfumo wa Hewa katika Idara ya Usimamizi wa tishio la Magonjwa ya milipuko na majanga wa WHO, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo.
Amesema “Mwaka huu umebainishwa na kuibuka na kuenea kwa kasi kwa aina mpya ya virusi vya AH3N2”.
Aina hiyo mpya inayoitwa J.2.4.1 au subkladi K amesema iligunduliwa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti nchini Australia na New Zealand, na tangu wakati huo imebainika katika zaidi ya nchi 30.
Mabadiliko ya kijenetiki ya virusi
Dkt. Zhang amesema “Takwimu za sasa za kitabibu hazioneshi kuongezeka kwa ukali wa ugonjwa, ingawa mabadiliko haya ya kijenetiki yanaashiria mageuzi muhimu ya virusi.”
Ameeleza kuwa virusi vya homa ya mafua hubadilika kila wakati, ndio sababu muundo wa chanjo ya mafua husahihishwa mara kwa mara.
“WHO hufuatilia mabadiliko haya, hutathmini hatari zinazohusiana na afya ya umma na kutoa mapendekezo ya muundo wa chanjo mara mbili kwa mwaka, kupitia mfumo wa kimataifa wa muda mrefu, Mfumo wa Ufuatiliaji na Hatua ya Mafua Duniani (GISRS) kwa kushirikiana na wataalamu wengine wa kimataifa,” amesema Dkt. Zhang.
Mtaalamu huyo wa WHO amefafanua kwamba Aina hiyo mpya haijajumuishwa katika muundo wa chanjo za hivi karibuni zilizotengenezwa kwa msimu wa mafua wa Ulimwengu wa Kaskazini,
Hata hivyo amesema “ushahidi wa awali unaonesha kuwa chanjo za msimu wa sasa bado zinatoa kinga dhidi ya magonjwa makali na hupunguza hatari ya kulazwa hospitalini.”
WHO inakadiria kuwa kuna takribani visa bilioni moja vya homa ya mafua ya msimu kila mwaka, vikiwemo hadi visa milioni tano vya ugonjwa mkali wa mfumo wa kupumua.
Kwa mujibu wa WHO Hadi vifo 650,000 kila mwaka vinahusishwa na magonjwa ya mfumo wa kupumua yanayotokana na mafua ya msimu.
Ushauri wa kupunguza hatari
“Chanjo bado ndio ulinzi wetu wenye ufanisi zaidi, ikiwemo dhidi ya aina zilizobadilika, hasa kwa makundi yaliyo katika hatari kubwa na wale wanaowahudumia,” amesisitiza Dkt. Zhang.
Mtaalamu huyo wa WHO amebainisha matokeo ya makadirio ya awali ya ufanisi wa chanjo dhidi ya aina mpya, yaliyochapishwa nchini Uingereza wiki chache zilizopita.
“Ni ya kutia matumaini,” amesema, akirejelea takwimu zilizoonesha kuwa chanjo ina ufanisi wa takribani asilimia 75 dhidi ya ugonjwa mkali na kulazwa hospitalini kwa watoto, na karibu asilimia 35 miongoni mwa watu wazima.
Dkt. Zhang ameonya kuwa msimu ujao wa sikukuu unaweza kuleta ongezeko zaidi la magonjwa ya njia ya upumuaji.
“Mipango ya mapema na juhudi za maandalizi, ikiwemo kuhamasisha upokeaji wa chanjo na kuimarisha utayari wa mifumo ya afya, zinapendekezwa kwa dhati,” amesema.
Ameshauri nchi kuimarisha uchunguzi wa kimaabara na ufuatiliaji wa magonjwa mwaka mzima, na kushiriki katika mtandao wa ufuatiliaji wa WHO wa GISRS.
Ufuatiliaji wa kimataifa bado ni muhimu
Mtandao huo unajumuisha vituo vya mafua katika nchi 130 pamoja na maabara kumi na mbili za marejeleo.
Alipoulizwa iwapo Marekani itaendelea kuwa mwanachama wa mtandao huo mwaka ujao licha ya uamuzi wa nchi hiyo kujiondoa WHO kuanzia tarehe 22 Januari 2026, Dkt. Zhang amesema kuwa, “kwa mtazamo wa mafua, ufuatiliaji wa magonjwa ya njia yamfumo wa hewa na maandalizi, bila shaka tunahitaji nchi zote duniani kushiriki katika ufuatiliaji, maandalizi na hatua kwa mafua na virusi vingine vya njia ya mfumo wa kupumuai, kwa sababu hatujui aina inayofuata ya janga, itajitokeza lini na wapi”.
Amehitimisha kwa kusema kuwa “Na muda kati ya kuibuka kwake na kugunduliwa, kuchambuliwa na kujumuishwa kwenye chanjo unaweza kuleta tofauti kubwa katika idadi ya maisha yanayoweza kuokolewa”.
♦ UN Source.









image quote pre code