Ticker

6/recent/ticker-posts

UTATA umeibuka kuhusu kifo cha Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ulyankulu



 UTATA umeibuka kuhusu kifo cha Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ulyankulu, Kaliua mkoani Tabora, Dk. Disma Chami, aliyetoweka siku 11 zilizopita baada ya mwili wake kukutwa porini.

Mwili wa daktari huyo umekutwa katika pori huko Kaliua, huku pembeni kukiwa na dawa mbalimbali za hospitalini.

Taarifa zilizosambaa mitandaoni mapema jana, zilieleza kuwa Dk.  Chami aliondoka nyumbani kwake Septemba 4, mwaka huu, akimuaga mke wake kuwa angerejea kesho yake.

Hata hivyo, hakurejea na alipotafutwa kupitia simu yake hakupatikana na ilipofika Jumatano ya wiki hii (Septemba 11) ilipatikana lakini kila alipopigiwa hakupokea.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa baada ya kutokupokea simu muda mrefu, inadaiwa kuwa alituma ujumbe mfupi kwa mke wake uliosomeka hivi, “Nisamehe sana, baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani, simamia kila kitu nilichokiacha pesa zote zipo CRDB bank, simamia watoto wasome kwaheri.”

Inaelezwa kuwa baada ya ujumbe huo, simu yake haikupatikana tena na Jeshi la Polisi lilimtafuta bila mafanikio na ndipo jana mwili wake uliokotwa maeneo ya Malolo ukiwa umechomwa sindano.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa pembeni mwa mwili huo kumekutwa na dawa mbalimbali za hospitalini ambazo zinadaiwa kutumika kujidunga au kudungwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, alipotafutwa na Nipashe ili kuzungumzia tukio hilo simu zake ziliita bila kupokewa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mganga huyo hakuuliwa, bali alijiua mwenyewe kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi kutoka Jeshi la Polisi.

“Yeye mwenyewe aliacha ujumbe akimtaka mke wake kulinda na kusimamia familia, hivyo tukio hilo halihusiani na kuuliwa.

“Hivyo utaratibu wa vipimo bado unaendelea, lakini ujumbe huo wamemkuta nao mke wake na kuthibitisha hilo.

“Jeshi la Polisi litakuja na taarifa rasmi kuhusu ni nani? Amekutwa wapi? Na vipimo vya kitabibu vinasema nini? Kuhusu kilichomkuta yote hayo yakiwa tayari umma utajulishwa baada ya madaktari kufanya postmortem (uchunguzi wa maiti).

Kuhusu madai ya kuwapo kwa mgogoro wa kifamilia kupitia taarifa za familia yake, Chacha alisema kuwa hakuna mgogoro wowote, kwani ujumbe ulioachwa haukuonesha.

Mkuu wa Mkoa huyo alisisitiza kwamba suala hilo linaendelea kuchunguzwa na hadi kufikia leo (Jumapili) majibu yatakuwa yamepatikana.

“Ieleweke kuwa hii ni taarifa ya mwanzo, kwani polisi na madaktari bado wanaendelea na uchunguzi, hivyo kama kutakuwa na taarifa kamili tutazitoa na kuueleza umma, ili kuondoa taarifa za upotoshaji zinazoendelea,” alisema Chacha.